Header Ads Widget

KANISA LA GILGAL CHRISTIAN MINISTRIES INTERNATIONAL LAZINDUA UJENZI WA KANISA LA WATOTO KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Kanisa la Gilgal Christian Ministries International lililopo Jijini Mwanza limezindua rasmi ujenzi wa jengo maalumu la kanisa la watoto, ikiwa ni hatua ya kuenzi na kukuza haki za watoto katika masuala ya kiimani.

Akizungumza katika ibada maalum ya wiki ya mtoto, Askofu Elias Sentozi wa kanisa hilo alieleza kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya maendeleo ya watoto iliyoanzishwa mwaka 2008, inayolenga kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.

“Tumeamua kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa vitendo kwa kuanzisha ujenzi huu ili watoto wapate sehemu yao maalumu ya kuabudu kwa uhuru, bila kuchangamana na watu wazima, huku vipaji vyao vikiendelea kulelewa na kukuzwa,” alisema Askofu Sentozi.

Sentozi aliongeza kuwa vipaji vya watoto havitokei vyenyewe bali vinahitaji kulelewa kwa kuwapa watoto fursa za kushiriki shughuli mbalimbali, ambapo hupatikana nafasi ya kubaini uwezo wao wa uongozi, kujiamini na kuelekeza wenzao.

“Tunawaandaa watoto hawa kuwa viongozi wa baadaye wa kanisa, serikali na jamii kwa ujumla. Maandalizi ya viongozi huanza kwa kuwajengea msingi thabiti wa kujiamini na uzalendo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Imma cate Foundation, Emmanuel Julius Ntobi, alitoa wito kwa jamii kutowatenga watoto wenye ulemavu kwa kuamini kuwa hawawezi kufanya mambo mbalimbali. Alisema watoto wote wanastahili fursa sawa za kukuza vipaji na kushiriki katika maendeleo ya jamii.

Baadhi ya wazazi walieleza kufurahishwa na uamuzi wa kanisa hilo kuanzisha wiki ya mtoto, wakisema hatua hiyo inawasaidia watoto kuelewa haki zao za msingi, huku pia ikiwajengea msingi wa maadili mema kupitia mafundisho ya kiroho.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Mwanza, Zena Kapama, alisema serikali inashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kuhakikisha watoto wanapata haki zao na malezi bora.

“Kuwajengea watoto kanisa ni hatua muhimu kwani watakuwa wanajifunza kwa uhuru kulingana na umri wao. Mmeendelea kuwafundisha maadili mema, ambayo yatasaidia taifa letu lenye changamoto ya kuporomoka kwa maadili kwa sasa,” alisema Kapama.

Kwa ujumla, hatua ya ujenzi wa kanisa la watoto imepokelewa kwa furaha na wadau mbalimbali wa maendeleo ya watoto, ikizingatiwa kuwa msingi wa maadili na hofu ya Mungu huanza kujengwa tangu wakiwa wadogo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI