Header Ads Widget

BRELA YASISITIZA UMUHIMU WA USAJILI RASMI WA BIASHARA KWA MAENDELEO YA MJASIRIAMALI

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma

WAKala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umehimiza wananchi, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, kuhakikisha wanasajili biashara zao kwa mujibu wa sheria, hatua itakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru, kupata mikopo, kulinda alama za biashara na kuaminika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA, Koyan Abubakari, alisema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kumsaidia mfanyabiashara si kumnyima fursa, na kwamba elimu ya usajili ndiyo silaha ya kwanza kwa maendeleo ya mjasiriamali yeyote.

“Tunawahimiza wananchi wote wa Dodoma na mikoa ya jirani wajitokeze kupata elimu ya usajili wa biashara, viwanda vidogo, alama za biashara pamoja na leseni. Hii ni hatua ya awali ya kujenga biashara imara na halali kisheria,” amesema Abubakari.

Aliongeza kuwa huduma zinazotolewa na BRELA katika maonesho hayo ni pamoja na usajili wa majina ya biashara kwa gharama ya shilingi 20,000, usajili wa viwanda vidogo, leseni za biashara na usajili wa alama za biashara (trade and service marks).

Aidha, wajasiriamali waliotembelea banda hilo wameelezea kufurahishwa na huduma wanazopatiwa Nzurika Zavala, mmoja wa wajasiriamali waliopata huduma ya usajili wa jina la biashara, alisema awali alitarajia urasimu, lakini alipokelewa kwa weledi na huduma ilitolewa papo kwa papo.

“Nimepewa cheti changu cha usajili bila usumbufu. Kwa kweli nimefurahi. Niliamini nitazungushwa lakini nimehudumiwa kwa haraka,” amesema kwa furaha.

BRELA ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki maonesho hayo kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi moja kwa moja, bila ya kulazimika kusafiri hadi ofisi kuu.

Kwa mujibu wa  Abubakari, BRELA itaendelea kutoa elimu ya mabadiliko ya kisheria yanayohusu biashara na leseni, ili kuhakikisha kila mwananchi anaelewa haki na wajibu wake katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi.

“Tunataka kila mfanyabiashara aondokane na dhana ya kufanya kazi kwa mazoea. Usajili si mzigo, bali ni kinga na njia ya kujijengea heshima ya kibiashara,” amesisitiza.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanaendelea hadi Juni 23, na wananchi wote wanakaribishwa kupata huduma mbalimbali za Serikali, ikiwemo usajili na elimu ya biashara kutoka BRELA.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI