Wakulima wa zao la kakao wilayani Kyela, mkoani Mbeya, wamehimizwa kuongeza thamani katika zao hilo ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa kaya zao na Taifa kwaujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephine Manase, wakati akifunga mafunzo ya kuongeza thamani ya zao la kakao, utafutaji wa masoko na uandaaji wa mipango ya biashara, yaliyoratibiwa na taasisi ya NMB Foundation.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Manase alieleza kuwa bado kuna fursa kubwa kwa wakulima kunufaika zaidi na zao hilo iwapo watajengewa uwezo wa kuchakata, kufungasha na kuuza bidhaa zenye thamani kubwa sokoni.
Kwa upande wake, Mratibu wa NMB Foundation Kanda ya Nyanda za Juu, Bw. Rodgers Shipella, alisema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi wa vikundi vya wakulima ili waweze kusaidia wenzao katika kuongeza tija kwenye uzalishaji wa kakao.
“Tunatambua umuhimu wa zao la kakao kwa uchumi wa wakulima wa Kyela. Ndiyo maana tumekuwa tukishirikiana na wadau wengine kuhakikisha elimu ya kuongeza thamani na biashara inawafikia kwa wakati,” alisema Bw. Shipella.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewapa mwanga mpya kuhusu namna bora ya kuboresha tija na mapato kupitia zao hilo.
Mafunzo hayo yalihusisha viongozi wa vikundi vya wakulima kutoka AMCOs 37 ambapo jumla ya wakulima 74 walipatiwa mafunzo ya siku nne kuhusu kuongeza thamani, utafutaji wa masoko na uandishi wa mipango ya biashara.
0 Comments