Header Ads Widget

VYEO SIO ZAWADI, NI MAJUKUMU ZAIDI – KAMANDA SENGA, SONGWE.

 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, amewakumbusha askari waliopandishwa vyeo kuwa vyeo hivyo si zawadi bali vinaambatana na ongezeko la majukumu katika kazi zao za kila siku.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 22, 2025, katika hafla ya kuwavisha vyeo jumla ya askari 62 waliopandishwa vyeo hadi ngazi za Koplo, Sajenti, Staff Sajenti na Sajini Meja. Askari hao walihitimu na kufaulu mafunzo ya vyeo kwa mwaka wa mafunzo 2024/2025. Zoezi hilo limefanyika katika Kituo cha Polisi Vwawa, Wilaya ya Mbozi, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura.

Kamanda Senga aliwataka askari hao kuvitendea haki vyeo vyao kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuheshimu mipaka ya kirafiki na undugu kazini, na kutokubagua au kuwa na muhali kwa mtu yeyote. Alisisitiza kuwa uadilifu na utii wa sheria ni misingi muhimu ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao ndani ya Mkoa wa Songwe.


Aidha, aliwasihi askari hao kujiandaa mapema kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya uchaguzi ujao, kabla, wakati na baada ya zoezi hilo, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu—kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI