Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba Dkt. Komba amewataka walimu waliopata mafunzo ya mbinu za kufundisha Kiingereza shuleni, kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata katika kuwawezesha wanafunzi kujifunza vyema darasani na kuifanya kazi hiyo kwa upendo.
Ameyasema hayo jana tarehe 28/05/2025 wakati akihitimisha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Uyui ya mkoani Tabora ambapo amesema kuwa mbinu walizopata walimu hao wanapaswa kuzitumia vyema katika kuwafundisha wanafunzi darasani.
“Hakikisheni mnawafundisha wanafunzi darasani kwa upendo na kisha mbinu mlizozipata mkazitumie vyema katika kuboresha kufundisha Kiingereza”amesema Dkt. Komba.
Amesema mafunzo hayo ya Kiingereza yataendelea baadae katika mikoa mingine ili kuhakikisha walimu wote nchini wanapata mbinu mpya ya kufundisha lugha ya Kiingereza vyema darasani.
Katika mafunzo hayo walimu, waliweza kufundishwa mbinu mbalimbali za ufundishaji Kingereza zenye kuwajengea ujuzi wa kutumia mbinu ya Jolly Phonics kukuza stadi za Kusoma na Kuandika (Literacy Skills) kwa Kiingereza kwa wanafunzi wa ngazi husika.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Tabora, Bwn. Pastory Mashiku amesema kuwa mafunzo hayo yataweza kusaidia walimu kwani wamepata ujuzi kutoka kwa wakufunzi mahiri jambo litakalowasaidia kwenye ufundishaji vizuri.
Akishukuru kwa niaba ya walimu wenzake, Mwenyekiti wa walimu katika mafunzo , Bw.Mashaka John amesema kuwa mafunzo yamewapa mwanga mzuri na kufahamu mbinu za ufundishaji wa Kiingereza na kuahidi kutumia vyema maarifa waliyoyapata na kuwapatia wenzao ambao hawakushiriki katika mafunzo.
Mafunzo yalianza tarehe 05/05/2025 katika vituo mbalimbali kwenye halmashauri 23 za za mikoa ya Rukwa, Iringa, Arusha na Tabora ambapo yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na kampuni ya Jolly Futures ya nchini Uingereza.
0 Comments