Header Ads Widget

SEKTA YA UCHUKUZI YACHANGIA DOLA BILIONI 2.48 BAJETI YA WIZARA YAPITISHWA

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma

SEKTA ya Uchukuzi nchini imeingiza dola za Marekani bilioni 2.48 za fedha za kigeni kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, sawa na ongezeko la asilimia 8.3 ikilinganishwa na dola bilioni 2.29 zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameyasema hayo akiwasilisha Bungeni Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Prof. Mbarawa amesema kuwa mapato hayo yanatokana na ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), pamoja na kodi nyingine zinazotokana na bidhaa kama mafuta ya petroli na dizeli. 

Aidha, taarifa ya mauzo ya huduma za usafirishaji hutolewa kwa pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika hatua nyingine, Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya shilingi trilioni 2.746 kwa mwaka wa fedha 2025/26. Bajeti hiyo inalenga kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kuboresha reli zilizopo, kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), pamoja na maboresho ya bandari, viwanja vya ndege, meli zilizopo na ujenzi wa meli mpya.

Waziri Mbarawa aliwashukuru wabunge 15 waliotoa mchango wao katika mjadala wa bajeti hiyo na kuahidi kuwa maoni na mapendekezo yao yatazingatiwa, hasa kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa safari za ndege za ATCL.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, ameipongeza Wizara hiyo kwa utekelezaji wa majukumu yake na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa mpango wa mwaka ujao wa fedha.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI