Na Shamila Rajab – Matukio Daima Media, Iringa
Mkurugenzi wa Makumbusho Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa katika Idara ya Utalii na Utamaduni, Jimson Sanga, amempongeza Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Iringa, Rita Kabati, kwa hatua yake ya kuibana serikali kuhusu kutangaza eneo la kihistoria la Kihesa Mgagao kuwa kivutio rasmi cha utalii wa kihistoria.
Sanga amesema kuwa hatua hiyo ni ya msingi sana katika kuimarisha sekta ya utalii mkoani Iringa, hasa kwenye maeneo yenye thamani ya kihistoria ambayo hayajapata kutangazwa ipasavyo licha ya umuhimu wake mkubwa.
“Mchango alioutoa mbunge wetu bungeni ni wa msingi katika kukuza sekta ya utalii mkoani Iringa, hasa kwa maeneo ya kihistoria ambayo bado hayajafahamika kwa wageni wengi.
Hatua hii si tu inasaidia kutangaza vivutio vya ndani, bali pia huongeza mapato ya taifa kupitia utalii, sambamba na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza sekta hii muhimu,” alisema Sanga.
Katika mchango wake bungeni jijini Dodoma, Mbunge Kabati aliitaka serikali kuongeza juhudi za kuboresha eneo la kihistoria la Kihesa Mgagao, akieleza kuwa ni sehemu muhimu kwa historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwani hapo waliishi na kufanyiwa mafunzo viongozi mbalimbali wa Afrika waliopigania uhuru wa mataifa yao.
Akiuliza swali la nyongeza, Kabati alisema:
“Kwa kuwa eneo la Kihesa Mgagao ni eneo ambalo waliishi marais waliopigania uhuru, na kwa kuzingatia kuwa wenzetu wa Afrika Kusini tayari wamejenga kivutio katika gereza alilowahi kufungwa Nelson Mandela, je, serikali ipo tayari kuongeza jitihada kuhakikisha kuwa eneo la Kihesa Mgagao linatangazwa rasmi na kuwa kivutio cha utalii nchini?”
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, alisema serikali tayari imepata ridhaa kutoka kwa wamiliki wa maeneo hayo, na kwamba hatua inayofuata ni kulitangaza na kuliboresha eneo hilo ili liingizwe rasmi kwenye orodha ya vivutio vya kihistoria vinavyotambuliwa kitaifa.
“Serikali imeshapata ridhaa kutoka kwa wamiliki wa maeneo hayo, na sasa kinachofanyika ni michakato ya ndani na mikakati ya kulitambua na kuliboresha eneo hilo kuwa urithi wa taifa nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira kwani suala hili lipo katika hatua za mwisho kukamilika,” alisema Kitandula.
Hatua hiyo imepongezwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, wakieleza kuwa itachochea ukuaji wa utalii wa ndani na nje pamoja na kuendeleza historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
0 Comments