Marekani imetia saini mkataba na Ukraine wa pamoja wa rasilimali zake za nishati na madini, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo yenye mvutano.
Nchi hizo mbili zimekubaliana kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa ujenzi ili kuchochea ufufuaji wa uchumi wa Ukraine kutokana na vita vyake na Urusi.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema ilionyesha pande zote mbili zimejitolea kudumisha amani na ustawi wa kudumu nchini Ukraine.
Kwa Kyiv, mpango huo unaonekana kuwa muhimu katika kupata msaada wa kijeshi wa Marekani.
Ukraine inaaminika kuwa na akiba kubwa ya madini muhimu kama grafiti, titanium na lithiamu. Uhitaji wa madini hayo ni mkubwa kwa sababu ya matumizi yake katika nishati mbadala, kijeshi na miundombinu ya viwanda.
Makubaliano hayo yanakuja huku kukiwa na vita vya kibiashara vya Marekani na China.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Wizara ya Fedha ya Marekani Jumatano alasiri, Mfuko mpya wa Uwekezaji wa Ujenzi mpya wa Marekani-Ukraine unatambua "msaada mkubwa wa kifedha na nyenzo" ambao Marekani imeipa Ukraine tangu Urusi ilipovamia Februari 2022.
Waziri wa Fedha wa Marekani alisema katika taarifa yake ya video kwamba mpango huo utasaidia "kufungua ukuaji wa Ukraine".
Taarifa hizo zinaonyesha mshikamano zaidi na Ukraine kuliko ilivyo kawaida katika utawala wa Trump.
Inarejelea "uvamizi kamili wa Urusi" na inaongeza kuwa "hakuna serikali au mtu ambaye alifadhili au kusambaza silaha kwa Urusi ataruhusiwa kufaidika na ujenzi mpya wa Ukraine".
Urusi bado haijajibu makubaliano hayo.
0 Comments