Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Devotha Minja, amesema uamuzi wa kususia uchaguzi unaoelezwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho si msimamo wa vikao halali vya chama, bali ni kauli binafsi za watu wachache ambao hawajafuata taratibu za ndani za chama.
Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi mkoani Morogoro, Devotha ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, amesema kuwa kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi kuhusu kususia au kuzuia uchaguzi hazijawahi kujadiliwa wala kupitishwa kwenye kikao chochote cha Kamati Kuu ya chama hicho.
“Leo CHADEMA imeamua kususia uchaguzi kwa maamuzi ya watu wachache, jambo hili halijajadiliwa wala kupitishwa na kikao chochote cha ndani ya chama. Mimi ni Mjumbe wa Kamati Kuu na natamka wazi kuwa hakuna kikao chochote kilichowahi kusema tunakwenda kususia uchaguzi,” amesema Devotha.
Ameongeza kuwa kaulimbiu ya No Reform No Election iliwahi kuzungumzwa ndani ya chama kama wito wa mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, lakini haijawahi kufikia hatua ya kutumika kama msingi wa kususia uchaguzi.
Amesisitiza kuwa CHADEMA ni chama cha kidemokrasia chenye taratibu, na kwamba maamuzi yoyote makubwa kama kususia uchaguzi lazima yapitishwe na vikao vya kikatiba.
0 Comments