Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Zulfat Muja, amewataka vijana mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kushiriki sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) ambazo zitafanyika kitaifa Mkoa wa Singida ili kumpa sapoti Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye atakuwa mgeni rasmi.
Akizungumza leo (Aprili 9, 2025) katika kikao cha Makatibu,Wenyeviti wa UVCCM na Makatibu hamasa wa wilaya zote za Mkoa wa Singida,amesema vijana wakijitokeza kwa wingi tutampa sapoti kubwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
"Tunayo Mei Mosi katika ugeni anakuja Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wetu wa CCM kwa hiyo sisi kama vijana wa Singida tuonyeshe kuwa tupo hai,tupo vizuri na tupo pamoja na zaidi tunamhakikishia ushirikiano," amesema Muja.
Muja amesema viongozi wa CCM wa Mkoa na viongozi wa serikali wa mkoa wamepongeza utulivu uliopo hivi sasa ndani ya UVCCM Mkoa wa Singida na wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa umoja huo ili uweze kutekeleza majukumu vizuri.
"Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata amefurahishwa na utulivu tulio nao na ametuahidi ataendelea kuupa umoja wa vijana ushirikiano, pia Mkuu wa Mkoa ametupongeza kwa namna ambavyo tumeendelea kuwa na ushirikiano wanaona ari mpya na nguvu mpya," amesema Muja.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa wa Singida amewaomba vijana kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kutekeleza majukumu ya kuijenga jumuiya hiyo na pale panapobidi kukosoana tukosoane kwa hekima na panapobidi kuambiana tuambiane kwa busara bila kudharauliana wala kutwezana.
"Mimi nilipo hapa sio kwamba najua yote hapana,lakinj nikiunganisha mawazo yenu na akili zenu ninaenda kufanikiwa na nitaendelea kuwa msikivu kwa wote na hili naendelea kukuomba Mungu sababu utulivu,upendo na ushirikiano ndio yatatufanya sisi Singida tuonekane na tufute makandokando ya nyuma yaliyokuwa yanatokea,"amesema Muja.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa ameongeza kwa kuwataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na mambo mazuri ambayo yataifanya UVCCM Mkoa wa Singida kuaminika na kuonekana na taswira mpya.
MWISHO
0 Comments