Tarehe 22 Aprili 2025, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wizara(Katiba na Sheria) na CHRAGG wamefanya kikao kazi kilicholenga kuishauri serikali kuandaa sera ya watetezi wa haki za binadamu nchini kwa malengo ya kuweka mazingira salama kwa wote wanaotetea na kulinda haki za binadamu nchini,
Upande wa THRDC,Kikao kiliongozwa na Afisa Programu kutoka Kitengo cha Kimataifa cha Huduma za Haki za Binadamu (ISHR)-Geneva, na Mshauri Mstaafu UN juu ya masuala ya uhuru na kujumuika ndugu Clemency Voule, Mratibu Taifa THRDC, na serikali ni wataalamu wa sera wakiongozwa na Mbaraka R. Stambuli, Mkurugenzi wa Sera na Mipango pamoja na Katibu Mkuu Wizara, ndugu Eliakim Maswi aliyehitimisha kikao hiki.
Wizara imepokea rasmi mapendekezo hayo na kupongeza THRDC kwa ushirikiano wake unaotumia taaluma ya sheria na ujuzi katika kukuza hali ya haki za binadamu nchini Tanzania.
Wizara imeiweka sera hii katika rejea muhimu na kuahidi kuitumia kikamilifu kwa masilahi mapana ya kitaifa ikiwa ni pamoja na hatua kadhaa ambazo Wizara imeushauri Mtandao kuendelea kupitia ili kufikia lengo hili Muhimu.
Wizara imeshauri kuhusisha masuala ya Watetezi wa haki za binadamu katika sera mbalimbali na mikakati inayoendelea kuandaliwa kwa sasa ikiwemo sera ya mfumo wa haki jinai na mpango kazi wa haki za binadamu na biashara.
Wizara pia , imependekeza kufanya marekebisho ya sheria zilizopo ili kushughulikia mapungufu ya sasa kama hatua ya awali katika kuwatambua na kuwapa ulinzi watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania.
Aidha, MoCLA na THRDC wamekubaliana kufanya ziara ya mafunzo katika nchi ambazo tayari zimepitisha sera au sheria hii na kupata uzoefu kwa ajili ya kuimarisha mchakato wa sera ya ulinzi wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania.
Kikao hiki kiliahirishwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, ambaye alisisitiza utayari wa Serikali kushiriki katika mchakato wa pamoja, jumuishi na unaozingatia maslahi ya Taifa katika kuimarisha ulinzi kwa watetezi wa haki za binadamu na Haki za Binadamu kwa ujumla.
Imetolewa na THRDC
22.04.2025.
0 Comments