Ibada ya mazishi ya Papa Francis inafanyika leo Jumamosi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambapo mamia kwa maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kuhudhuria, wakiwemo viongozi wa dunia, familia za kifalme na maafisa wa Kanisa Katoliki.
Shughuli ziitaanza saa 10:00 kwa saa za huko sawa na saa 7 mchana kwa saa za Afrika Mashariki na inatarajiwa kudumu kwa karibu saa moja na nusu. Baada ya misa kumalizika, mwili wa Francis utasafirishwa hadi katika kanisa la Santa Maria Maggiore mjini Roma kwa mazishi. Baada ya hap Kipindi cha maombolezo cha siku tisa kitaanza.
Viongozi mbalimbali mashuhuri waliothibitisha kuhudhuria ni pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mfalme Felipe VI na Malkia Letizia wa Uhispania, Rais Lula da Silva wa Brazil, na Prince William kwa niaba ya Mfalme Charles III.
Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na mkewe Melania wapo miongoni mwa wageni wa heshima, hii ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi katika muhula wake wa pili. Trump alimwelezea Papa kuwa “mtu mwema aliyewapenda watu wanaopitia magumu.”
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer naye yupo mjini Vatican, akimtaja Papa Francis kama “kiongozi jasiri aliyejitolea kwa maskini na waliosahaulika.”
Brazil, nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi duniani, ilitangaza siku saba za maombolezo kitaifa, huku Rais Lula akimkumbuka Papa kama sauti ya haki na usawa duniani.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasili kuhudhuria, Mkewe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine pia wamewasili. Viongozi wengine wanaohudhuria ni pamoja na Rais wa Poland Andrzej Duda, Rais wa Argentina Javier Milei, Rais wa Italia Sergio Mattarella, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Papa Francis alifariki dunia Jumatatu, Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88. Alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Rome kwa muda kutokana na matatizo ya kupumua yaliyochochewa na maambukizi ya homa ya mapafu.
0 Comments