Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amekipongeza kituo cha afya Nyasho kwa kupata tuzo ya utoaji huduma bora za afya kwa mwaka 2025 kwa ngazi ya kituo cha afya.
Licha ya kukipongeza kituo hicho pia ameipongeza zahanati ya kwangwa kwa kupata tuzo ya utoaji wa huduma bora kwa mwaka 2025 kitaifa kwa ngazi ya zahanati.
Akizungumza na Matukio Daima leo april 9,2025 kwa njia ya simu kutoka bungeni jijini Dodoma amesema tuzo hizo zilizotolewa na Wizara ya afya zinaonyesha namna huduma nzuri zinavyotolewa ndani ya jimbo la Musoma mjini.
Amesema waganga na wauguzi kwenye kituo cha afya Nyasho na zananati ya Kwangwa wanahitaji pongezi kwa kazi nzuri na kupelekea kupata tuzo hizo.
Mathayo amesema hilo ni jambo kubwa kwa kuwa Wizara ya Afya kupitia ufatiliaji wake imeona huduma bora zinazotolewa maeneo hayo na kuamua kutoa tuzo hizo.
Amesema afya ni suala la msingi na amefarijika kuona wananchi wanapewa huduma bora za afya kwa kuwa ni jambo jema.
" Nichukue nafasi hii kuwapongeza wahudumu wa afya kwenye kituo cha afya Nyasho na zahanati ya Kwangwa kwa kutoa huduma bora za afya kwa mwaka 2025.
" Lakini pia nimpongeze mkurugenzi wa manispaa ya Musoma na mganga mfawidhi wa manispaa kwa usimamizi wao mzuri wa huduma za afya",amesema.
Mbunge huyo amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wahudumu wa afya kwenye vituo vya afya,zahanati na hospitali zilizopo jimbo la Musoma mjini.
0 Comments