Header Ads Widget

MAVUNDE AZINDUA KIWANDA CHA BARUTI NA VILIPUZI CHA SOLAR NITROCHEMICALS LTD.

 

Na  Matukio Daima Media Kisarawe.

WAZIRI wa Madini Antony Mavunde amezindua kiwanda kikubwa nchini cha uzalushaji wa baruti na vilipuzi cha Solar Nitrochemicals Ltd  chenye thamani ya shilingi bilioni 19.


Mavunde amezindua kiwanda hicho kilichopo Kijiji cha Visegese Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha baruti na vilipuzi na kuongeza pato la sekta ya madini.


Amesema kuwa mahitaji ya baruti hapa nchini ni tani 26 ambapo kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 22 kwa mwaka huku uwezo wa kuzalisha vilipuzi ni milioni 15 na mahitaji ni vilipuzi milioni 10 na nchi itaelekea kuacha ununuzi wa vilipuzi toka nje ya nchi.


"Sekta ya madini ambapo mwaka 2023 ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 7.2 na mwaka 2024 liliongezeka na kufikia asilimia tisa na mwaka huu malengo ni kufikia asilimia 10,"amesema Mavunde.


Aidha amesema hii ni historia na anamshukuru Rais kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo serikali itashirikiana na wawekezaji ili nchi ipate mafanikio kupitia sekta hiyo ya madini.


Kwa upande wake mwenyekiti wa kampuni Milind Desmukh amesema kuwa kitatoa ajira za moja kwa moja kwa watu 300 na za muda zitafika hadi 1,000 kwa miaka ijayo.


Desmukh amesema kuwa mbali ya uzaliahaji pia kitasaidia kuwapatia utaalamu kwa wafanyakazi na kuwapatia ujuzi na kusaidia viwanda vya ndani na kuuza nje ya nchi.


Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema kuwa changamoto iliyopo kwenye eneo hilo la Visegese ni maji na barabara na kuiomba serikali kukabili hali hiyo ili kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.


Magoti amesema kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya viwanda ambapo anashukuru uwekezaji huo kwani umetoa ajira kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo mengine.


Naye Diwani wa Kata ya Kazimzumbwi Adam Ngimba amesema kuwa asilimia 70 ya ajira ni vijana kutoka Kisarawe ambapo kiwanda kinachangia maendeleo ya Kata hiyo.


Ngimba amesema kuwa kuhusu maji zimebaki kilometa tatu ili maji kufika kwenye eneo hilo ili kuondokana na changamoto hiyo na barabara wanasubiri fidia ili ujenzi uanze.

mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI