Header Ads Widget

JARIBIO LA MAPINDUZI YA DR CONGO: WAMAREKANI WALIOFUNGWA MAISHA JELA WALIRUDISHWA NYUMBANI


 

Wamarekani watatu waliopatikana na hatia kwa kuhusika katika mapinduzi yaliyofeli nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwaka jana wamerudishwa nyumbani Marekani kutumikia kifungo kilichosalia.

Watatu hao awali walihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi kabla ya hukumu zao kubadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela wiki iliyopita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Tammy Bruce alisema watatu hao "wako chini ya ulinzi wetu".

Hatua ya kurejeshwa nyumbani inawadia wakati Marekani na DR Congo zikifikia makubaliano ya madini katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.

Wiki iliyopita, mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump katika bara la Afrika alitembelea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuthibitisha kuwa nchi hizo mbili ziko kwenye mazungumzo kuhusu madini na kusema inaweza kuhusisha "uwekezaji wa mabilioni ya dola".

DR Congo ina akiba kubwa ya madini ya coltan na cobalt, yanayotumika katika vifaa vya kielektroniki na betri za magari ya umeme, ambayo kwa sasa yanachimbwa kwa kiasi kikubwa na makampuni ya uchimbaji madini ya China.

Wafungwa watatu wa Marekani - Marcel Malanga Malu, Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin - waliondoka DR Congo Jumanne kutumikia kifungo kilichosalia nchini Marekani, alisema msemaji wa rais wa Congo Tina Salama.

Walisindikizwa hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'Djili mjini Kinshasa "kwa kufuata taratibu za kisheria", ilisema urais wa DR Congo.

Uhamisho huo "ni sehemu muhimu ya kuimarisha diplomasia ya mahakama na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya haki na haki za binadamu" kati ya DR Congo na Marekani, ofisi ya rais iliongeza.

Wamarekani hao walikuwa miongoni mwa watu 37 waliohukumiwa kifo Septemba iliyopita na mahakama ya kijeshi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI