Matanki ya kuhifadhia maji katika mradi wa maji wa Mtego wa Noti wilaya ya Uvinza mkoa Kigoma
Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa dhana ya baadhi ya watu kuwa huduma ya maji safi na salama inayopatikana baada ya miradi kukamilika kuwa inapaswa kuwa ya bure ndiyo chanzo cha kukwamisha miradi mingi ya maji kushindwa kuwa endelevu katika utoaji huduma.
Andengenye amesema hayo akizindua mradi wa maji katika kijiji cha Mtego wa noti kwenye mji mdogo wa Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa wananchi wanapaswa kulipia uendeshaji wa miradi ya maji iliyokamilika ili huduma iweze kuwa endelevu kwa muda mrefu.
Katika uzinduzi huo Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne serikali imeleta mkoani Kigoma kiasi cha shilingi Bilioni 429 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji nia ikiwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na makazi ya watu ili kuondoa usumbufu wa kutumia muda mwingi na kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo wa Mtego wa Noti Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Uvinza, Mhandisi Bakari Kiwitu amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni moja kimetumika katika utekelezaji wa mradi huo wenye lengo la kupeleka huduma kwa wakazi 9448 wa vijiji vya Mtego wa Noti na Mganza.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa UNICEF mkoa Kigoma, Justus Ndenzako alisema kuwa Shirika hilo limetoa fedha kiasi cha shilingi Milioni 952.6 kupitia mfuko wa Poul Due Jenson, Grundfos ikiwa ni sehemu ya shilingi Bilioni 9.2 ambazo Shirika ilo limechangia miradi ya maji mkoani Kigoma ambapo wananchi wa vijiji hivyo viwili wamechangia kiasi cha shilingi milioni 47.6.
Mwisho.
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji kijiji cha Mtego wa Noti wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
Mkuu wa UNICEF mkoa Kigoma, Justus Ndenzako akitoa salam za shirika hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Mtego wa Noti wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Meneja wa RUWASA wilaya Uvinza Bakari Kiwitu (kulia) akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Mtego wa Noti kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye (kushoto).
0 Comments