Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAKATI Chama cha mpira wa miguu nchini (TFF) kimevifungia viwanja vitatu nchini kwa kukosa sifa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimeviita vilabu vya ligi kuu nchini kutumia uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma kama uwanja wake wa nyumbani..
Katibu wa siasa,uenezi na mafunzo CCM mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo alisema kuwa wakiwa wamiliki wa uwanja huo wanazialika timu za ligi kuu na ligi daraja la kwanza (Championship) kuutumia uwanja huo kwani uko vizuri na usalama wa kutosha.
Nsokolo alisema kuwa CCM mkoa Kigoma itaendelea kuusimamia na kuimarisha vigezo vilivyowekwa na TFF ili kuhakikisha uwanja unakidhi vigezo wakati wote ili uweze kuchezewa na kueleza kuwa kusimamia na kuendeleza michezo nchini ni moja ya mambo yaliyopo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hivyo watahakikisha uwanja huo unakuwa upo vizuri wakati wote hivyo timu itakayotumia uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma haitajutia uamuzi wake huo.
Kwa upande wake Meneja wa uwanja huo Shaban Rajabu maarufu Shaban Buti alisema kuwa amekuwa akifanya jitihada kubwa kuhakikisha uwanja huo unakuwa na vigezo vilivyowekwa na TFF ndiyo maana miaka mingi uwanja huo umekuwa ukitumika bila kufungiwa.
Buti alisema kuwa kutokana na kazi kubwa anayofanya amepata tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Meneja bora wa mwaka kwa mwaka 2024 jambo ambalo limemti moyo kuhakikisha analinda heshima hiyo na heshima ya CCM mkoa kuhakikisha uwanja unakuwa vizuri wakati wote.
Mapema wiki hii Chama cha Soka nchini (TFF) imevifungia viwanja vya CCM Kirumba Mwanza, Ally Hassan Mwinyi Tabora na Liti cha Singida kwa kukosa vigezo vya kuchezewa mashindano ya Ligi kuu nchini.
Mwisho
0 Comments