Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa CCM mkoani Kigoma kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa viwango vinavyokubalika na kuleta tija kwa wananchi.
Majaliwa ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa mkoa Kigoma alisema hayo wilayani Kakonko mkoani Kigoma katika kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa CCM ambayo kimkoa yanafanyika wilayani humo na kubainisha kuwa serikali imetoa fedha nyinyi mkoani humo hivyo ni lazima fedha hizo zilete matokeo katika Maisha ya wananchi.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Livingstone Lusinde (Kibajaji) Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa Zaidi ya shilingi Trilioni 11.4 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hivyo viongozi wa CCM wanalo jukumu la kuitembelea,kuikagua, kuisemea miradi hiyo.
Awali Akitoa taarifa ya mkoa Katibu wa CCM mkoani Kigoma, Christopher Pallangyo alisema kuwa hali ya chama mkoani humo imeimarika na imeshinda nafasi za serikali za mitaa kwa asilimia 96 na kwamba wana uhakika uchaguzi wa mwaka huu wa madiwani, wabunge na Raisi watafanya vizuri.
Pallangyo alisema kuwa wana ushirikiano mkubwa na serikali ya mkoa huo ambayo inatekeleza miradi mbalimbali kutokana na kiasi vccha shilingi Trilioni 11.4 ambazo serikali imepeleka kutekeleza miradi na kwamba Kigoma imepiga hatua kubwa kwenye maendeleo kutokana na kutekelezwa kwa miradi hiyo ikiwemo ya barabara ambapo kwa sasa mradi wa barabara ya kiwango cha Lami kutoka Kigoma hadi Nyakanazi kilometa 360 kinakaribia kukamilika huku sehemu kubwa ya barabara hiyo ikipitika kwa lami.
Naye Mkuu wa wilaya Kakonko Evance Mallasa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kuwa serikali chini ya usimamizi wa CCM imefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa miradi ya wananchi.
0 Comments