Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea na mikutano mbalimbali ya wananchi mkoani Kigoma imefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa ndoa baina ya wanandoa wawili katika Kijiji cha Rumashi wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma baada ya wanandoa hao kunyimana huduma kwa miaka minne.
Usuluhishi huo umekuja baada ya Mwana Mama Dativa Kachira kujitokeza mbele ya wanasheria na wataalam wanaoshiriki kutoa huduma kwenye kampeni hiyo wilayani Kakonko na kueleza madhira na changamoto zinazomkabili ikiwemo mume wake Stides Stephano kukataa kutoa matumizi ya nyumbani ya familia wala kugharamia huduma za elimu za Watoto wao hivyo familia kukabiliwa na hali ngumu.
Mwanamke huyo alisema kuwa Mume wake ana uwezo wa kuhudumia faamilia na kuweza kuishi vizuri lakini hali imekuwa mbaya hivyo kumlazimu kufik kwenye uongozi wa serikali mara kwa mara kumshitaki lakini bado hakuna hatua Madhubuti ambazo zilichukuliwa kumfanya mwanaume huyo ahudumie familia.
Akijibu hoja na tuhuma zilizoelekezwa kwake mbel ya wanasheria na wataalam wanaoshiriki kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mwanaume huyo alisema kuwa mke wake ndiyo alianzisha mgogoro kwa kuwafukuza nyumbani Watoto aliokuwa amezaa na mke wake wa kwanza lakini amekuwa akinyimwa chakula na huduma nyingine nyumbani hapo.
Sambamba na hilo Stephano alisema kuwa mke wake aliuza mazao yote waliyolima na hakumpatia hata sentimoja na katika fedha wanazopokea kutoka kwenye mpango wa kata masikini anapaswa kupata shilingi 10,000 kila mwezi lakini hajawahi kupokea hata senti moja kwani pesa zote zinapitia kwa mke wake ambaye anatumia peke yake.
Kufuatia ushauri waliopewa na wanasheria wa Kampeni ya msaada wa sheria ya Mama Samia ikiongozwa na Mratibu wa wilaya Kakonko, Jackline Kulwa wanaondoa hao walikubali kusameheana kwa yote yaliyotokea na kuahidi kuishi Pamoja kwa amani na kukutunza familia yao huku wakipeana mikono na kuombana msamaha.
0 Comments