Header Ads Widget

VIWANDA VYATAKIWA KUTUMIA MALIGHAFI ZINAZOZALISHWA NCHINI.


 VIWANDA nchini vimetakiwa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini ili kulinda wawekezaji kwani soko la ndani ndiyo ustawi wa uwekezaji nchini.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Waziri wa Ujenzi Abdala Ulega wakati akifunga maonyesho ya nne ya Biashara na Uwekezaji Mkoani Pwani.

Ulega amesema kuwa uwepo wa uwekezaji wa viwanda ni sehemu ya ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo wamiliki wa viwanda hawana sababu ya kuagiza malighafi za uzalishaji bidhaa toka nje ya nchi.

"Wenye viwanda watumie malighafi zinazozalishwa hapa nchini na tujivunie bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili wawekezaji wawe na uhakika wa soko kuanzia la ndani na baadaye la nje,"amesema Ulega.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa suala la upungufu wa umeme litakwisha kwani vyanzo vya umeme vimeongezeka.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Pwani Mkuu wa Wikaya ya Mkuranga Hadija Nasir amesema kuwa wanaomba bajeti ya miundombinu ikiwemo ya umeme, maji na barabara iongezwe ili kuwarahisishia wawekezaji.

Naye Mkurugenzi wa TCCIA Oscar Kisanga akizungumzia kuhusu sekta binafsi amesema wao ni daraja kati ya wafanyabiashara na serikali ambapo maonyesho hayo ni sehemu ya kujitangaza na kupata masoko.

Maonyesho hayo yalihusisha wafanyabiashara na wawekezaji kuonyesha bidhaa wanazozalisha yalianza Desemba 16 na yamemalizika leo Desemba 20.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI