NA WILLIUM PAUL, SAME.
TAMASHA la utalii la Same utalii festival limezinduliwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro ambapo limetajwa kama chanzo cha kuibua na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika wilaya hiyo.
Pia tamasha hilo limechangia kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo ambapo awamu ya kwanza imepelekea wawekezaji watatu kuwekeza kwa kujenga hoteli za kisasa za utalii.
Akizungumza leo wa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu Katibu Tawala wa mkoa huo, Kiseo Nzowa alisema kuwa tamasha hilo ambapo kwa mwaka huu ni awamu ya pili limekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa.
Alisema kuwa, mbali na kutangaza vivutio hivyo tamasha hilo pia limekuwa likikuza mzunguko wa biashara kupitia wageni mbalimbali ambao hufika katika wilaya hiyo kufanya matumizi pia kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu maswala ya utalii.
"Tamasha hili la Same utalii festival linasaidia kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika wilaya ya same pia limesaidia vivutio vilivyopo kutambuliwa rasmi kama mali kale na Vivutio vya utalii" Alisema Katibu Tawala Nzowa.
Aliongeza kuwa, wilaya ya Same ilikuwa inatambulika kama wilaya isiyo na vivutio vya utalii lakini kupitia tamasha hilo limeonyesha vivutio vingi vinavyopatikana Same.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema kuwa, lengo la tamasha hilo ni kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kutangaza utalii kupitia kampeni yake ya Royal tour ambayo imeleta mafanikio makubwa kwa kuongeza watalii nchini.
Kasilda alisema kuwa, lengo jingine ni kuhakikisha vivutio vya utalii vilivyopo Same vinawanufaisha wananchi wa wilaya hiyo pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa kupitia utalii.
"Moja ya fanikio kubwa ambalo tumelipata kupitia awamu ya kwanza ni kuwapata wawekezaji watatu ambao wanakuja kujenga hoteli za kisasa tatu katika wilaya yetu ambapo itapelekea vijana kuzalisha ajira kupitia uwekezaji huo" Alisema Kasilda.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, kwa sasa idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana same imeongezeka mara mbili ambapo imechangia kukuza vipato vya wana same.
Mwisho..
0 Comments