NA MARYAM HASSAN
WAKATI umefika sasa Zanzibar kuondokana na dhana kuwa nafasi za wanawake viti maalum kuwa ni za watu aina fulani pekee na badala yake lazima uwepo ukomo wa kuondosha suala hilo.
Tumeshuhudia kwamba wapo baadhi ya wanawake wameshikilia nafasi hizo enzi na enzi hali ambayo inawafanya kudumaa kuwa wao nafasi yao yao ni viti maalum pekee.
Mafunzo mbali mbali yanatolewa kutoka taasisi na wanaharakati ili kuwawezesha wanawake hao kuondokana na mawazo mgando waliyonayo juu ya nafasi hizo na badala yake kutoka walipo na kuingia katika majimbo ili kuonesha umahiri wao kwa kuwa tayari wameshajifunza mbali mbali ya uongozo.
Lakini tunashuhudia kwamba wanawake hao wamekuwa na hofu kubwa ya kuingia katika majimbo kwa kuwania nafasi za uwakilishi au ubunge na badala yake kuwa na mawazo mgando ambayo yanawafanya kushindwa kuchukua maamuzi hayo.
Vyama vya siasa, wanaharakati wa haki za binadamu bado wana kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wanawake hawa kuhakikisha sasa wanatoka katika nafasi walizo nazo na kuingia katika majimbo.
Leo tunamzungumzia Mwanaidi Kassim Mussa mwanamke anayepania kufanikiwa katika siasa na kuleta mabadiliko katika jamii ambae sasa anaeleza kuwa wakati umefika yeye kuingia katika jimbo kuonesha uwezo wake.
Akiwa na maono ya kuwa kiongozi mwenye kusukuma maendeleo, Mwanaidi anaonyesha uwezo wake wa kuleta mwamko mpya katika siasa za vijana na wanawake.
MAISHA YA AWALI
Mwanaidi Kassim Mussa alizaliwa katika kijiji cha Migombani wilaya ya Mjini, mama wa watoto wa wanne , mwenye umri wa miaka (52),kati ya hao watatu wanaume na mmoja ni mwanamme ambae amekulia katika familia ya kawaida, ambapo maisha hayakuwa rahisi.
Akiwa shuleni, alikuwa miongoni mwa wanafunzi walioonesha uwezo mkubwa wa kujadili masuala ya kijamii, na ndoto yake ya kuwa kiongozi ilianza kujengwa tangu hapo.
NDOTO ZA UONGOZI
Mwanaidi alilelewa na wazazi wake wawili yaani Baba na Mama aliweka malengo ya kuingia katika siasa ili aweze kupaza sauti za watu wasio na uwezo wa kujieleza.
“Nataka kuleta mabadiliko, siyo kwa ajili yangu tu, bali kwa jamii yangu na hasa wanawake na vijana ambao wanakumbana na vikwazo vingi,” alisema.
MAONI YA MAMA
Mama yake, Habiba Mustafa Ali,(69) anasema kuwa Mwanaidi alikuwa na ndoto ya kuwa kiongozi tangu akiwa mtoto.
“Alikuwa na tabia ya kushirikiana na wenzake katika masuala ya uongozi, kwenye jumuiya ya Umoja wa vijana youth liague akiiga wanasiasa wa wakati huo.
Alikuwa msikivu na mwenye hamasa ya kusaidia wengine, na hilo limekuwa sehemu ya maisha yake hadi leo,” alisema mama yake kwa furaha.
MAONI YA MUME
Kwa upande wa mume wake,Hassan Haji Hassan anasema: “Nimemwona mke wangu Mwanaidi akijituma sana kufanikisha ndoto zake, na nimemshauri aingie katika majimbo kwa sababu uwezo anao mkubwa” alisema.
Kila siku anafanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo yake na kuwasaidia watu katika jamii yetu, namhakikishia kuwa nitakuwa nae bega kwa bega, ili kuhakikisha kuwa anapiga hatua na najivunia sana kumuona akipiga hatua.”
ELIMU NA MAENDELEO
Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari, Mwanaidi alipata fursa ya kujiunga jumuiya ya umoja wa vijana Kisiwandui na kugombea nafasi mbali mbali za chama kwa miaka tofauti.
SAFARI YA KUINGIA KATIKA JIMBO IFIKAPO 2025
“ Nia yangu ni kuingia katika majimbo lakini nashindwa kwa sababu bado kunachangamoto ambazo naziona kupitia kupitia viongozi waliopo baadhi yao wamekuwa na mpasuko” alisema Mwanaidi.
Anaeleza kuwa mpaka sasa uwezo anao kwa sababu tayari ameshahudumu nafasi ya viti maalum kwa muda wa vipindi vitatu , hivyo alisema atahakikisha kupitia uchaguzi wa 2025 anajitosa katika jimbo ambalo hakupenda kulitaja.
Mwanaidi anaeleza anatarajia kutoka nafasi aliyopo na kuingia katika majimbo ili nafasi ya viti maalum itawaliwe na wanawake wengine.
Anafahamisha kuwa majimbo mengi hivi sasa yanatawaliwa na waunaume hivyo wakati umefika kwa wanawake ambao tayari wamepata mafunzo na kuhudumu nafasi za viti maalum kuhakikisha wanaingia katika majimbo kwa sababu uwezo wanao,pia kuongeza idadi ya wanawake katika majimbo.
Mwanaidi anaeleza kuwa wapo baadhi ya wanaume hawajawa tayari kuwaunga mkono katika nafasi hizi na badala yake wanaendeleza mfumo dume kuwa mwanamke hawezi kuongoza.
Hivyo aliwataka wanawake kuonesha msimamo kwa kuwaunga mkono wanawake wenzao kwa sababu ya wingi uliopo na wananafasi kubwa ya kushinda katika majimbo.
HITIMISHO
Kwa bidii na maono yake makubwa, Mwanaidi amejidhihirisha kuwa mwanamke kijana anaeweza kuleta mabadiliko.
Akiwa na msaada wa familia, marafiki, na jamii inayomzunguka, anaendelea kusukuma mbele ndoto yake ya kuwa kiongozi mkubwa wa kisiasa.
Sauti yake itakuwa muhimu katika kusaidia kundi la vijana na wanawake kujiamini na kushiriki katika uongozi wa taifa,kwa kuwa tayari ameonesha nia thabit kuwa anaweza kuwa kiongozi bora.
0 Comments