Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Duru zimeeleza kuwa maendeleo yote yanayopigwa nchini yanachagizwa na uwekezaji katika elimu na hivyo ni lazima mkazo katika sekta hiyo uongezwe kwa kujenga miundombinu bora itakayozalisha wataalamu wazuri.
Katika harambee ya ujenzi wa bweni la wavulana katika chuo cha Aman chini ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Kusini Njombe Naibu waziri wa viwanda na biashara Exaud Kigahe aliyemwakilisha waziri wa fedha amesema hatua ya Kanisa kujenga chuo hicho inasaidia sana kukuza uchumi wa Taifa kupitia wasomi wanaozalishwa.
Taarifa ya ujenzi wa Bweni hilo iliyosomwa na Katibu mkuu wa KKKT Dayosisi ya kusini Njombe Imeeleza kuwa Jumla ya shilingi Bilioni 1.1 zinahitajika ili kukamilisha mradi huo na kwamba kwa hatua za awali zinahitaji zaidi shilingi milioni 500 huku Askofu wa Dayosisi ya Kusini Dokta George Fihavango akisema vyuo vinasaidia kusisimua uchumi wa mkoa na kukuza elimu.
Baadhi ya wadau wa elimu mkoani Njombe akiwemo Eliud Nyauhenga aliyekuwa meneja wa Mfuko wa Barabara Nchini na Deo Mwanyika mbunge wa jimbo la Njombe mjini wamesema suala la elimu sio la kulifumbia macho kwa namna yoyote kwani watoto ni lazima wasome.
Baada ya Harambee hiyo Naibu waziri huyo akatangaza kupatikana kwa zaidi ya shilingi milioni 100.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi mkoani Njombe wamepongeza hatua ya kanisa la KKKT Kufikiri kujenga Hosteli za wavulana kwani itawasaidia kuepukana na gharama za kuishi mitaani.
0 Comments