Header Ads Widget

TAMKO LA LHRC KUHUSU KUKAMATWA KWA ALIYEKUWA MEYA WA UBUNGO BONIFACE JACOB


  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza masikitiko yake kuhusu kukamatwa kwa aliyekuwa Meya wa Ubungo, Ndugu Boniface Jacob, tukio ambalo limetokea leo, Septemba 18, 2024, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kupitia mashuhuda na mawakili wake, mazingira ya ukamataji wa Bw. Jacob hayakufuata taratibu za kisheria kama zinavyotakiwa na sheria za nchi, jambo lililosababisha taharuki kwa umma. LHRC inabainisha kuwa hili ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya ukamataji usiofuata sheria ambao umeongezeka kwa kasi, huku mamlaka zinazohusika zikiendelea kukaa kimya bila kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu na taratibu zinazotumika.


Kukamatwa kwa Bw. Jacob kunafuatia msururu wa matukio ya kutisha yanayolenga wanaharakati wa haki za binadamu, hususan wale wanaotumia mitandao ya kijamii kuhoji na kukosoa mamlaka za serikali. Matukio haya yamezua hofu na wasiwasi mkubwa katika jamii, hasa kwa wale wanaojitolea kupigania haki za raia na uwajibikaji wa serikali.


LHRC imesisitiza kwamba Tanzania, kama nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, inapaswa kuheshimu haki za kila raia, ikiwemo haki ya kuishi kwa amani, uhuru wa kujieleza, na ulinzi wa kisheria. Kukithiri kwa vitendo vya ukamataji kiholela na utekaji kunatoa picha ya udhaifu katika utawala wa sheria, hali ambayo inavunja misingi ya haki za kikatiba zilizotajwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan haki ya kuishi, haki ya ulinzi, na uhuru wa kujieleza bila hofu wala vitisho.


Matendo Haya Ni Ukiukaji wa Sheria


Kamata kamata ya watetezi wa haki za binadamu inaashiria ukiukaji wa wazi wa Katiba ya Tanzania na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za binadamu. LHRC inatoa wito kwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa haki, usawa, na demokrasia vinahifadhiwa kwa manufaa ya jamii yote. Kukamatwa kiholela na kutoweka kwa raia kumechukua sura mbaya, na sasa ni wakati muafaka kwa mamlaka kuchukua hatua madhubuti kurekebisha hali hii.

LHRC pia inatoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua zifuatazo:

1. Kutoa Maelezo Sahihi Kuhusu Kukamatwa kwa Bw. Jacob: Vyombo husika vinapaswa kufafanua kwa kina tuhuma zinazomkabili Bw. Jacob na kuhakikisha kuwa uchunguzi unafanyika kwa uwazi na kufuata misingi ya haki.

2. Kuhakikisha Taratibu za Kisheria Zinafuatwa: Sheria na taratibu za ukamataji zinapaswa kufuatwa ipasavyo ili kuzuia taharuki na hofu kwa raia. Ripoti za vitendo vya utekaji vinavyofanywa na watu wanaojitambulisha kama polisi zimekuwa zikiongezeka, jambo ambalo linakiuka taratibu sahihi za ukamataji kama zilivyoainishwa kwenye sheria.

LHRC imeahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama ya Ndugu Boniface Jacob ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na sheria zinafuatwa kikamilifu.

Imetolewa na:

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)


Dkt. Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI