Header Ads Widget

KERO YA UBOVU WA BARABARA MKIMBIZI WANANCHI WAPAZA SAUTI DIWANI AWATULIZA




Mwendesha boda boda Mkimbizi akipita katika barabara ya Mkimbizi ambayo ni kero kubwa.


NA MATUKIO DAIMA APP 

WANANCHI  wa Kata ya Mkimbizi, mkoani Iringa, wamelalamikia ubovu wa barabara yao na kutoa wito wa kuharakishwa kwa ujenzi wa lami katika barabara hiyo.

 Wanasema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa mji wa Iringa, kwani inatumika sana kusafirisha bidhaa za kilimo na biashara nyingine zinazochangia pato la wananchi na maendeleo ya kijamii.


Wakizungumza Leo na Matukio Daima Tv wakzi wa  kata hiyo walisema hali ya sasa ya barabara ni mbaya, hasa wakati wa mvua, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa kwa magari na watu wanaotumia barabara hiyo. 

"Tunapata hasara kubwa kwa kuchelewa kufikisha mazao sokoni, na magari yetu yanaharibika mara kwa mara," alisema mmoja wa wananchi hao.


Wananchi hao waliikumbusha serikali juu ya ahadi zake za awali za kuboresha miundombinu hiyo. 

Walisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa mji wa Iringa, hasa kutokana na umuhimu wake katika kuunganisha kata hiyo na maeneo mengine ya mkoa.


Matukio Daima Tv tumemtafuta Diwani wa Kata ya Mkimbizi, Eliud Mvela kwa njia ya simu ambao amesema kuwa barabara hiyo ipo katika mpango wa ujenzi wa lami kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 na tayari mchakato umeanza kwa kufanya upembuzi yakinifu.


Alisema kuwa ujenzi wa Barabara hiyo unajengwa wa Benki ya Dunia hivyo wananchi  wawe na Imani na kuwa mchakato wa ujenzi umeanza kwa hatua za awali kwa kufanya upembuzi yakinifu na kabla ya mwaka 2025 itakuwa tayari.

Alisema kuwa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kiuchumi katika Manispaa ya Iringa hivyo kukamilika kwake ni Ukombozi wa maendeleo ya kata hiyo na Mtwivila .

"shida ya barabara ni kubwa sana Mkimbizi hata Mimi mwenyewe najua hivyo napambana kuona ujenzi inafanyika "


Hata hivyo Mvela amewatuliza wananchi kwa kusema kwa kuwa  tayari mipango ya ujenzi wa barabara hiyo imeanza wawe na Imani na serikali .

 Alifafanua kuwa barabara hiyo imepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.

Diwani Mvela aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuanza kabla ya mwezi januari mwakani2025.


Barabara ya Mkimbizi-Mtwivila, iliyopo katika mji wa Iringa, ni mojawapo ya miundombinu muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni katika eneo hilo.

 Barabara hii ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha shughuli za biashara, kilimo, usafirishaji, na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wakazi wa Iringa na maeneo ya jirani. 

Hivyo, kuiboresha barabara hii kwa kiwango cha lami ni hatua muhimu kwa maendeleo ya mji wa Iringa na kwa ustawi wa wananchi wake.

Barabara ya Mkimbizi-Mtwivila inatumika sana kwa ajili ya usafirishaji wa mazao ya kilimo, bidhaa za  mbali mbali na huduma za kibiashara. 

Iringa ni miongoni mwa mikoa inayotegemea kilimo kama chanzo kikuu cha uchumi, na barabara hii ni njia kuu ya kusafirisha mazao kwenda kwenye masoko ya mjini na nje ya mkoa. 

Wakulima hutumia barabara hii kusafirisha mazao kama mahindi, viazi, na mboga kutoka mashambani hadi sokoni. 

Ikumbukwe kuwa ubovu wa barabara unawafanya wakulima wengi kuchelewa kufikisha mazao yao sokoni, jambo linalosababisha hasara, huku wengine wakishindwa kabisa kusafirisha kutokana na gharama kubwa za usafiri.

Barabara hii ni kiungo muhimu kati ya wafanyabiashara wa maeneo ya vijijini na miji mingine. 

Kupitia barabara hii, bidhaa za kibiashara hupatikana sokoni, hivyo kuchangia pato la taifa na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi. 

Iwapo itajengwa kwa kiwango cha lami, kutakuwa na ongezeko la biashara na uwekezaji katika sekta ya usafirishaji na huduma, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji wa Iringa na mkoa kwa ujumla.

Pia mji wa Iringa ni kitovu cha utalii wa kihistoria na wa mazingira, ukiwa na vivutio kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo ya kihistoria ya Kalenga. 

Hivyo barabara ya Mkimbizi-Mtwivila ina mchango muhimu katika usafirishaji wa watalii wanaotembelea vivutio hivi kutoka mikoa ya Kaskazin na Kanda ya kati Dodoma kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha bila kupita katikati ya mji wa Iringa.

Ili shughuli za utalii vikue zaidi kumbuka watalii wengi hutoka nje ya mkoa na nchi, wanahitaji miundombinu bora ya usafiri ili kufika kwenye vivutio hivyo kwa urahisi na usalama.

Kama ubovu wa barabara utabaki hivi utaathiri mtiririko wa watalii, jambo linalopunguza mapato yanayotokana na sekta ya utalii. 

Ujenzi wa lami kwenye barabara hii utaboresha hali ya usafiri, hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaofika Iringa, jambo ambalo litachangia uchumi wa eneo hilo kupitia malazi, chakula, usafirishaji, na huduma nyingine zinazotolewa kwa watalii.

Barabara ya Mkimbizi-Mtwivila ni kiungo muhimu kwa wakazi wa kata ya Mkimbizi, Mtwivila, na maeneo mengine ya jirani.

 Barabara hii hutumiwa na wanafunzi wanaokwenda shule  za msingi na Sekondari ya Mtwivila pia wagonjwa wanaohitaji matibabu, na wafanyakazi wanaosafiri kwenda maeneo ya kazi kila siku. 

Hivyo hali mbaya ya barabara inasababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa maeneo haya, hasa wakati wa mvua ambapo barabara huwa haipitiki.

Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami utarahisisha usafiri wa watu na bidhaa, hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile elimu, afya, na maji safi.

 Wananchi wataweza kufika katika shule, hospitali, na maeneo mengine muhimu kwa urahisi na kwa muda mfupi. 

Aidha, itapunguza gharama za matengenezo ya magari na usafiri wa umma ambao sasa Mkimbizi umetoweka kabisa kutokana na kero ya barabara  jambo linalowafanya  kwa  wananchi kutumia fedha zao nyingi kwenye usafiri na kuacha shughuli nyingine za maendeleo.

Ubovu wa barabara mara nyingi huongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali za barabarani, hasa kutokana na madereva kushindwa kudhibiti magari yao kwenye barabara zenye mashimo na maji yaliyotuama. 

Ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utasaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa, kwani magari yatakuwa yanaendeshwa kwenye barabara yenye usawa na yenye kuhimili hali ya hewa.

Hakuna ubishi kuwa arabara nzuri huongeza usalama wa raia kwa kuwaondoa kwenye maeneo hatarishi yanayoweza kusababisha ajali au kuwa sehemu za uhalifu. 

Mwangaza mzuri na ulinzi wa kutosha unaweza kuwekwa kwenye barabara zilizo bora, jambo ambalo litaongeza usalama wa watu wanaosafiri usiku au nyakati za asubuhi mapema.

Barabara ya Mkimbizi-Mtwivila ni daraja muhimu linalounganisha mitaa na maeneo ya mjini. 


Wakazi wa mitaa wanategemea barabara hii kuingia mjini kwa ajili ya kutafuta huduma mbalimbali na kuuza mazao yao. 

Hivyo barabara ikiwa mbovu, kunakuwa na vizuizi vya kiuchumi na kijamii kati ya vijiji na mji, jambo ambalo linaathiri maendeleo ya kijamii.

Ujenzi wa lami kwenye barabara hii utaimarisha usafiri kati ya Mkimbizi na Mtwivila na maeneo mengine ya mji wa Iringa pia wageni wataweza kupita Kihesa Kilolo kuingia Mkimbizi ,Mtwivila Zizi la Ng'ombe hadi Kitwiru iwapo daraja la Kitwiru litajengwa kwa wakati .

Kwa ujumla, barabara ya Mkimbizi-Mtwivila ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni katika mji wa Iringa. Ujenzi wake kwa kiwango cha lami ni hatua itakayoboresha ustawi wa wakazi wa eneo hilo kwa kurahisisha usafiri, kuimarisha biashara na kilimo, kuchochea utalii, na kuboresha huduma za kijamii.

Hivyo  Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuharakisha ujenzi wa barabara hii ili kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkimbizi, Mtwivila, na maeneo ya jirani ambao wapo mjini ila kero ya barabara inawawakumbusha Vijijini walikozaliwa.


MAKALA HII IMEANDIKWA NA FRANCIS GODWIN MTAYARISHAJI WA MAUDHUI MATUKIO DAIMA MEDIA 0754026299KWA HABARI NA MAKALA MBALI MBALI ENDELEA KUFUATILIA MATUKIO DAIMA APP,MATUKIO DAIMA BLOG NA MATUKIO DAIMA TV (ONLINE) PIA MITANDAO YOTE YA KIJAMII NA USIKOSE KUSOMA GAZETI LA MWANAHABARI NA MACHINGA KILA SIKU AMA SOMA GAZET LA DIRA MAKINI KILA JUMATATU NA ALHAMIS IWAPO UNAHITAJI KUTANGAZA NASI PIGA SIMU 0754026299 EMAIL: matukiodaima3@gmail.com

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI