NA WILLIUM PAUL, SAME.
ZAIDI ya shilingi milioni 152 zimetumika kuwasha Umeme kwenye Kijiji cha Mvaa kata ya Bombo wilayani Same mkoani Kilimanjaro ambapo kufika kwa nishati hiyo kijijini hapo kunafanya wilaya hiyo kusalia na Vijiji tisa (9) pekee ambayo havijafikiwa na huduma ya Umeme kati ya Vijiji mia moja (100) vinavyounda Wilaya hiyo.
Wakizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo wakazi wa Kijiji cha Mvaa wamekiri kuunganishwa na huduma ya Umeme kwenye nyumba zao, ambapo wameishukuru Serikali kukamilisha mradi huo kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiitamani huduma hiyo pasipo na mafaniko.
Semu Mmamba, ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki amesema mbali na kukamilika kwa mradi huo lakini kumekuwa na ushirikiano mzuri baina ya Shirika la Umeme nchini TANESCO Wilaya ya Same na Ofisi ya Mbunge hali ambayo imesaidia kuimarika kwa huduma Jimboni hapo na kupunguza malalamiko ya wananchi juu ya TANESCO.
Kwaupande wake Menaja wa TANESCO wa Wilaya hiyo, Mhandisi Fabian Ruhumbika amesema hadi sasa wateja 67 wameunganishwa na huduma hiyo kati yao zikiwemo taasisi za umma na binafsi, huku akisema kwa upande wa vijiji tisa vilivyo salia tayari Serikali kupitia Wakala wa Nishati vijijini REA Same imeshamleta Mkandarasi yupo site kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuanza kazi ya kufikisha Umeme kwenye maeneo hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ambaye ndiye mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mradi huo amesema kufika kwa Umeme Kijijini hapo ni sehemu ya uboreshaji wa huduma za kijamii kama Hospitali, Vituo vya Afya na zahanati lakini pia njia moja wapo ya wananchi kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza pia wakazi wa Bombo kutumia fursa ya kufika kwa nishati hiyo vizuri ili iweze kuwa na tija kwao, pamoja na kulinda miundombinu yake isihujumiwe ili huduma iwe endelevu.
“Kukamilika kwa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi CCM lakini pia ni safari ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ifikapo mwezi Desemba 2025 vijiji vyote vya Same vitakuwa vimefikiwa na Umeme" Alisema Kasilda.
Na kuongeza "pongezi zangu nyingi zimfikie Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kwa namna ambavyo anawapambania wananchi wake kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana karibu na jamii lakini pia Menejimenti ya TANESCO na REA Same kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi CCM”.
0 Comments