Header Ads Widget

DKT. MWAKAJUMILO, PROF. LUMUMBA WAKUTANA KENYA KUIJENGA AFRIKA.


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Ukombozi wa Fikra Afrika (UWAFIA) Dkt. Stephen Isaac Mwakajumilo, amekutana na kufanya mazungumzo na Prof. PLO Lumumba jijini Nairobi nchini Kenya na kuzungumza mambo mbalimbali kwa ajili ya kuhimiza mwamko na maendeleo ya bara la Afrika.

Ziara ya Dr. Stephen Isaac Mwakajumilo, mwanzilishi na Mwenyekiti wa Ukombozi wa Fikra Afrika (UWAFIA), inakuja kufuatia mwaliko wa Prof. PLO Lumumba ambaye pia ni Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya PLO Lumumba kwa muda mrefu ikiwa lengo kuu ni kujadili masuala ya Ukombozi wa Fikra za Waafrika.

Katika kikao hicho wawili hao wamekubaliana kushirikiana katika kuhimiza wananchi kujitambua na kujiamini kuwa wananchi wa bara la Afrika wanaweza kufika mbali kimaendeleo kutokana na raslimali mbalimbali juu ya ardhi ya Africa.

Dkt. Mwakajumilo amesema Afrika ni tajiri kwani ina ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo, mbuga za wanyama, madini, bahari, mito na maziwa na raslimali nyingine ambazo zikiratibiwa na kuboreshwa vizuri zinawezawasaidia zaidi kiuchumi hususani bidhaa za mazao kuongezewa thamani badala ya kuongezwa thamani yakisafirishwa nje ya nchi.

Dkt. Mwakajumilo ambaye ni msomi wa masuala ya uchumi, amesema ni lazima bara la Afrika liungane kujenga uchumi ili kujiimarisha badala ya kutegemea nguvu ya mataifa ya ughaibuni pekee katika kuinua uchumi wao wakati wana raslimali nyingi.

Mara kwa mara Dkt. Stephen Isaac Mwakajumilo ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mbeya na mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara amekuwa akihimiza jamii kujitambua na kujisimamia kwa kubadili mtazamo na fikra ili kufikia maendeleo endelevu na ukombozi wa Afrika kutoka uhuru wa bendera hadi kuwa na uhuru wa kiuchumi, kisiasa na nyanja nyingine zote.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI