Header Ads Widget

BABA WA ALIYECHOMA PICHA YA RAIS SAMIA ALIA NA KUTEKWA MWANAYE, AOMBA KUSAIDIWA.

 NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Baba mzazi wa kijana Shadrack Chaula (24) aliyedaiwa kuchoma picha ya Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mzee Yusuph Chaula (56) amewaomba wananchi na Serikali kuendelea kumsaidia kumtafuta mwanaye aliyetekwa na watu wasiojulikana tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti 2024.

Mzee Chaula amesema hayo kwenye mahojiano maalum na kituo hiki nyumbani kwake kitongoji cha Mapanga kijiji cha Ntokela Ndanto Tukuyu wilayani Rungwe.


Ameomba kijana wake huyo ambaye ni msanii wa uchoraji, mfanyabiashara na mjasiriamali arejeshwe ama akiwa hai au amekufa.


Amesema ikiwa anadaiwa wadai watalipwa na ikiwa ana kosa lolote basi afikishwe kwenye vyombo vya sheria.


Pia Chaula amewashukuru viongozi, wanaharakati na wananchi kwa ujumla waliomchangia kijana wake huyo na kumtoa jela kwenye kosa la awali la kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuhukumiwa na mahakama kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi million tano.


Hivi karibuni, kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, alieleza kuwa Polisi ilishaanza uchunguzi wa tukio hilo la utekaji na kutoa mwito kwa mtu au watu wenye taarifa za mahali alipo kijana Shadrack kutoa kwa familia, Serikali au kwenye vituo vya polisi.


Kijana Shadrack Yusuph Chaula alidaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Agosti 02, 2024 akiwa kwenye biashara yake ya nguo kijijini Ntokela ambapo watu watatu wasiofahamika walifika na gari ndogo na kumchukua ghafla na kutokomea naye kusikojulikana uelekeo wa Mbeya mjini kutoka wilayani Rungwe na mpaka sasa hajapatikana hivyo familia na vyombo vya dola vinaendelea kumtafuta.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI