NA THABIT MADAI,ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA APP
MGOGORO wa Muda Mrefu katika Kanisa la Anglikana Zanzibar umechukua Sura mpya baada ya Wazee, Wajumbe wa Halmashauri ya Mtaa na Wakristo wa Kanisa Kuu la Mkunazini pamoja na Mbweni wametoa Tamko la kutaka kujitenga kutokana na maamuzi yaliyofikiwa na kikao kilichoitishwa na Askofu Mkuu Dkt Maimbo Mndolwa ambacho kiliazimia kumrudisha Kanisani hapo Askofu Michael Hafidhi.
Aidha, wamepinga uhalali wa kikao hicho pamoja na wamamuzi yote yaliyotolewa kutokana na kikao ambacho wanadai kuwa ni batili na kusema kuwa kwa sasa hawatapokea maelekezo yoyote kutoka Makao makuu ya Kanisa hilo Dodoma.
Akitoa Tamko leo mbele ya Waandishi wa Habari kwa niaba ya Wazee, Wajumbe wa Halmashauri ya Mtaa wa Wakristo wa Kanisa la Kuu la Kristo Mkunazini na Mbweni, Mzee wa Kanisa la Mkunazini Mwalimu Jane Sudi amesema kwamba, kikao kilichoitishwa Mnamo tarehe 30 Agost huko mbweni na Askofu Mkuu Maimbo Fabian Mndolwa ni kikao batili ambacho kilikuwa na adhma ya kuligawa kanisa hilo.
"Tukiwa katika Ombwe hili la Muda Mrefu, Siku ya Jumatano Tarehe 30 Agost 2023 Askofu Mkuu Dkt Maimbo Fabian Mndolwa alifika Zanzibar na kufanya kikao na wajumbe ambao hawana nguvu kikatiba ya kufanya maamuzi yoyote katika Dayosisi," Ameeleza.
"Askofu Mndolwa aliwapa Ajenda Wajumbe na kuwataka kupiga Kura jambo ambalo ni kinyume na taratibu,kanuni na katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania na Katiba ya Dayosisi ya Zanzibar," ameongeza.
Amefahamisha kwamba, kutokana na Mgogoro huo Msimamo wao ni kuiomba Halmashauri ya Kanisa Kuu ya kuanza haraka utaratibu wa kujisajili kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.
"Sisi Wazee Waanglikana hapa Zanzibar tumeumizwa na sana kuhuzunishwa na mambo yanayoendelea ambapo inaonesha huko Dodoma wanatupuuza, tunaishauri Halmashauri ya Kanisa kuu ianze haraka utaratibu wa kujisajili kwa Mujibu wa Sheria za Zanzibar ili kulinasua kanisa," ameeleza.
Amefafanua kuwa, kuanzia siku ya leo hawatapokea maelekezo yoyote kutoka Dodoma wala kwa Askofu Mkuu Dkt Maimbo Mndolwa.
"Waanglikana wa Zanzibar tunao uwezo wa kujiongoza wenyewe, tutajisimamia wenyewe kama ilivyo kwa Ofisi ya Mufti kwa ndugu zetu Waislamu ambapo hawahitaji Bakwata kuwasimamia," Amefafanua.
Mgogoro katika Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Zanzibar umeibuka baada ya Wakristo wa Kanisa hilo kumshtaki Askofu Michael Hafidhi kwa makosa ya Ukosefu wa Maadili, Ubadhirifu wa Mali za Kanisa na Matumizi mabaya ya Madaraka ya Ofisi ya Askofu.
0 Comments