Header Ads Widget

MBUNGE PROF. PATRICK NDAKIDEMI AHUDHURIA MAHAFALI YA SHULE YA MSINGI SINGA CHINI MAZOEZI.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ambaye ni mhitimu kutoka  Shule ya Msingi ya  Mazoezi  Singa Chini  ameshiriki mahafali ya darasa la saba katika shule hiyo.


Mbunge Prof. Ndakidemi aliyesoma shuleni hapo hadi darasa la saba alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo ambapo aliungana na wanafunzi waliosoma hapo na kumaliza elimu ya msingi mnamo  mwaka 1973 ambao walikuwa na kumbukizi ya miaka hamsini tokea wahitimu. 



Mwenyekiti wa Wahitimu hao, Adrian John Mushi alieleza kuwa wamechanga fedha na kulipia zaidi ya shilingi milioni  2.7 kwa shirika la umeme Tanzania ili kuingiza umeme shuleni hapo.



Shughuli zilianza kwa wanafunzi, wazazi pamoja na wageni wengine kuhudhuria ibada ya misa kumshukuru Mungu kwa watoto waliohitimu darasa la saba mwaka huu na wale waliomaliza elimu ya msingi miaka 50 iliyopita. Katika ibada hiyo, Padri Evaristi Miku aliwapongeza wahitimu hao kwa kuikumbuka shule iliyowalea na kuwajengea msingi wa maisha.


Akizungumza katika hafla hiyo Mwalimu Mkuu  alieleza changamoto kubwa hapo shuleni ni pamoja na Uchakavu wa nyumba ya mwalimu mkuu pamoja na ukosefu wa nyumba za waalimu, ukosefu wa Umeme na Wazazi kutochangia michango ya chakula cha mchana kwa wanafunzi hali inayopelekea kuwepo utoro wa wanafunzi pamoja na uchakavu ya miundombinu ya maji ikiwemo mabomba, na matenki ya kuhifadhi maji.



Akiongea katika mahafali hayo, Mbunge Ndakidemi aliwaasa wazazi kutoa michango ya chakula kikamilifu kwani hiyo ndiyo nyenzo kuu na siri kubwa ya  wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao. 

Kuhusu kero ya nyumba za kulala na miundombinu ya maji, aliwaomba wadau wa maendeleo waendelee kutoa michango ili kwa pamoja watatue kero hizo ambapo alitoa mchango wa shilingi milioni moja kwa ajili ya kutandaza waya katika madarasa na ofisi za waalimu ili waweze kupatiwa umeme, utakaosaidia kurahisisha masomo na shughuli za TEHAMA.



Mbunge alikabidhi vyeti vya kuhitimu kwa wanafunzi wa darasa la saba na kutoa tuzo mbalimbali kwa waliofanya vizuri katika elimu, nidhamu na uongozi.



Sherehe za mahafali na kumbukizi hiyo zilihudhuriwa na wageni mbali mbali wakiwemo Diwani wa Kata ya Kibosho Mashariki Christopher Ndakidemi,    Padre Evaristi Miku wa Kanisa la Mtakatifu Patris Singachini, Masista, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Singa Chini , walezi wa shule pamoja na wazazi wa wahitimu.



Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI