Na Simon Joshua - Matukio Daima App, Zanzibar.
Zainab Mtima ni mmoja wa madereva ambao watakufikisha salama lakini licha ya kufikia kiwango hiki cha kuwa dereva mwanamke na dereva maarufu visiwani Zanzibar, amepitia mengi magumu na ya kukatisha tamaa.
Dunia ni darasa tosha kwa kila mwanaadamu na changamoto za maisha ndio sehemu ya maisha yenyewe hapa ulimwenguni, baadhi ya watu hukumbana na changamoto katika maisha yao mpaka kufikia kukata tamaa ya kuishi kwenye ulimwengu huu na kuona bora kifo kwao kuliko kuishi.
Wapo wengi wenye mawazo kama hayo ambayo huwajia baada ya kukutana na mitihani aidha iwe ndani ya ndoa yake, au nyumbani kwao au kazini au kwenye jamii na hapo huamua lolote ambalo lipo kichwani kwake huliamua bila ya kujali kama lina madhara au lina faida katika maisha yake. Na huamua kufanya jambo lolote lile iwe lina muelekeo au halina liwe linafanana naye au halifanani muhimu maisha yaendelee.
Akielezea faida alizopata anasema kwanza ni kupata kazi ya uhakika na aliyokuwa mwenyewe ameikubali, pili ni kupata umaarufu mkubwa wa kuwa dereva wa taxi pekee hapa Zanzibar, tatu amejenga heshima badala ya kutukanzwa sasa anaheshimika, nne amekuwa anakubalika anapoomba msaada anasaidiwa bila ya manyanyaso na pia amekuwa na kampuni yake ya Zain Women Tour&travel Agency.
“Pia kazi imenifanya nikamilishe nguzo tano za Uislamu nimekwenda hijja pamoja na shida zote nilizopata lakini nimepata fedha za kwenda kuhiji Makka Alhamdulillah,” alishukuru.
“Wito wangu kwa wanawake wanapopatwa na mitihani wasipagawe bali wapambane kuhakikisha wanatimiza malengo yao, jambo la msingi wawe na subira ili wafanikiwe” alimalizia kwa kuwashauri wanawake wenzake.
Hali kama hiyo iliwahi kumkumba Zaynab Khamis Mtima (Zainab Mataxi) anayejulikana kwa jina la “The Queen of Steering” ambaye alikumbana na changamoto za maisha ya kila namna katika ndoa na mwisho akaishia kufanya kazi ambayo hakuitarajia katika maisha yake.
Zaynab ni mama wa watoto watatu ameolewa na mdogo na amehatika kupata watoto watatu, Hassan, Hussein na Hassanat lakini maisha ya ndoa aliyopitia yamempa funzo kubwa na kumfanya awe jasiri zaidi kutokana na changamoto alizozipitia na kutaka iwe mfano kwa wengine ili wanapokumbwa na matatizo wasivunjike moto bali wajikaze kibwebwe na kusonga mbele kwani waamini kwamba matatizo ni sehemu ya maisha na mwanamke hatakiwi kuvunjika moyo.
Zaynab kielimu ana degree ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam na safari yake ya maisha yake ilianza pale tu alipoanza kupata changamoto za ndoa, Zaynab aliolewa vyuo zaidi ya vitatu na kupata changamoto mbali mbali na changamoto hizo ndio zilizofungua fursa na akili yake ikakomaa na kupata fursa ya kuzigeuza zile changamoto kuwa ndio shule yake nyengine iliyomfunza namna ya kujikwamua kimaisha na kuendelea na maisha yake.
“Na sababu kuu ya kuanza kuyumba na kupepesuka kimaisha ni pale nilipoachwa ndoa yangu ya tatu, ilikuwa sijamaliza chuo, sina mtaji wa kufanya biashara yoyote ile, sikuwa na sehemu ya kuishi na maisha yalikuwa magumu sana sina fedha na sina chochote huku nasoma na huku nina watoto maisha yalikuwa mazito sana lakini nashukuru walimu wangu wa chuo wakanishauri nisiache chuo, na kunambia changamoto ni za kupita lakini taaluma yako itabakia milele, hapo nikapata moto na nikasema naweza kusonga mbele”.
Na kuongeza kwamba “Niliachwa kabla sijamaliza chuo nilikuwa na wakati mgumu mno yaani siyosahau katika maisha yangu yote, maana mwaka wa kwanza wa chuo mama yangu Bi Rehema Mfaume Kawawa alipata ajali mbaya sana na akalazwa Hospital ya Tumbu Kibaha na hali ikazidi kuwa mbaya tukahamishiwa Hospitali ya Muhimbili lakini sijakaa sawa kero za ndoa zikaanza mwaka wa pili muhula wa kwanza mume aliniacha na kunipeleka polisi” alisema Zainab na alijikhisi kama kachanganyikiwa na maisha.
Hata hivyo Zainab hakukata tamaa kipindi hicho nilipoteza mume na baadhi ya marafiki zake na wale ambao walikuwa naye hawakuwa na uwezo wa kumsaidia na hivyo alipiga konde moyo wake akaona ajitahidi kutafuta lile ambalo litakuwa na afuweni ili asonge mbele kwenye maisha.
Baada ya kuona maisha yameanza kuwa magumu na amekuwa ombaomba jambo ambalo hakuweza kuliepuka kutokana na hali aliyokuwa nayo na huku akijiuliza ataendelea hadi lini katika hali hiyo ya kuombaomba ndipo lilipomjia wazo la kuanza kujifundisha gari ambapo hakuwa na mtaji wowote wa kuanzisha biashara akafikiria wazo la kujua uendeshaji wa gari kwanza akaanza kujifunza udereva.
“Sina mtaji wowote, naishi kwa kuomba msaada, na hakuna kitu kibaya ambacho sikipendi kama kuomba mahitaji ya kila siku wakati nina nguvu na uwezo wakufanya kazi, lakini maisha na hali ngumu ya kiuchumi ilinilazimu kuwa ombaomba” aliongea huku akiongesha kuchukizwa na hiyo hali.
Anasema akapata ujuzi wa kuendesha gari lakini hakuwa na gari ya kuendesha ambayo wazo lake lilikuwa ni kuendesha watu ili apate fedha za kujikimu baada ya kufikiria kila kitu cha kufanya lakini bila ya mafanikio.
Aliwafuata watu mbali mbali na kuwaomba wampe gari ili afanye biashara ya kuchukua abiria lakini alikumbana na changamoto mbali mbali na kuambulia matusi na maneno mabaya kila upande na hivyo jambo hilo lilikaribia kumkatisha tama lakini akasema siwezi kukata tama bali akasonga mbele na kutafuta watu wengine ili wamsaidie.
“Huwezi amini zoezi hilo pia nilikwama na kupata majibu yasiyoridhi na baadhi yao waliniambia hiyo kazi ya kiume, wengine wakanambia hiyo kazi ya kihuni na tena hata ndugu zangu kaka zangu wenye uwezo wana magari mawili mawili basi waliishia kunibeza na kunishangaa kwamba kazi gani ya utaxi driver si ya mwanamke” alisema!
anasema watu wengine anamjibu huku anapanda gari lake kwa kejeli na kumuacha na mshangao, lakini baada ya kukosa msaada kote ndipo alipopata maarifa mengine mapya, akenda bandarini kuwatafuta wahusika, akajielezea mmoja alimpokea ingawa alipigwa vita na madereva wenziwe.
“Huyo jamaa alinambia Zaynab tulia hapa utakuwa mpiga debe wangu, ukijaza gari napeleka abiria nikirudi nakupa pesa yako” alisema huku akionesha furaha
Kwa mara ya kwanza akaanza kazi ya kupiga debe pale lakini siku ya kwanza hakupata abiria hata mmoja akarejea nyumbani akiwa na huzuni hakuwa na furaha na akakosa hata nauli ya kumrejesha nyumbani.
“Nilirudi nikiwa siamini kama kuna siku nitapata abiria na niweze kupata pesa, nikawa nafikiri nyumba yenyewe nimesaidiwa tu na watu wananisaidia chakula cha watoto wangu lakini najiuliza moyoni jee nitagaiwa chakula kila siku mapaka lini” aliwaza huku akijiuliza wakati akirudi nyumbani anasema.
Aidha alikumbana na changamoto za madereva wa kiume ambao walikuwa wanahofia kupoteza ajira zao wakidai kuwa Yule mwanamke uwepo wake pale utasababisha wanawake wengi kufanyakazi ya udereva taxi huku wengine wakadai yeye ni usalama ametumwa pale ende kuwachunguza madereva kila mmoja alikuwa na chuki yake dhidi ya Zaynab na wengine walipendekeza afukuzwe nisifanye kazi pale kabisa ambapo yeye mwenyewe alingangania na hakukubali kushindwa akiwajibu kwamba hakuna wa kumfukuza na hata akifukuzwa hataondoka.
“Nimepata tabu sana mimi walikuwa wananiambia wewe mwanamke usituletee balaa unataka kuleta mambo ya kuhamasisha wanawake wa Zanzibar wawe madereva wa texi sio? Wengine wakinambia mimi nimetumwa kuja kufanya mambo ya kuwachunguza wakiniita mimi ni usalama wa taifa lakini wakanifukuza na hapo ndio nikapanda hasira nikawajibu sendi popote na mkinitimua patachimbika hapa” alisema huku akitabasamu.
Na nikawaambia nakumbuka kama wiki hivi wakapigiana simu waje kituo kimevamiwa na mwanamke, hiyo siku palichimbika nikawaambia kuwa hapa kila mmoja amekuja kutafuta rizki yake. Kama kuna asiyenitaka miye hapa Basi atoke yeye, Nakama hamuamini atakayethubutu kunitoa ajue hiki kijiwe kitakufa hatobaki mtu hapa.
Kila shida alipata ya kutukanwa na kuitwa majina mabaya na kukaingia fitana kubwa akifitinishwa ili asipewe gari ya kufanyia kazi lakini hakuvunjia moja akaendelea kwenda bandarini Malindi kupiga dege ili apate fedha huku kwa siku akipewa shilingi 500 pekee kwa siku na kuna baadhi anaondoka na shilingi 1000 siku nzima.
Akaendelea na kupiga debe na huku anatafuta tajiri ampe kazi ya kuendesha gari yake kwa kuwa alishachoka kupiga hivyo akafanikiwa kupewa gari ya abiria inayotoka mjini kwenda Kinuni, “Nakumbuka gari ishajaza nataka kuondoka abiria wakagoma kuendeshwa na miye, yule tajiri wa gari mke wake ndio akamwambia mumewe akanipatie gari ndogo kwa rafiki yake” alisema huku akicheka.
Alifanya kazi vizuri alipopata gari ndogo lakini bahati mbaya gari ikauzwa, akatafuta nyengine kwa bahati kuna Jumuiya moja ikajitokeza kumsaidia gari akafika mpaka kujaza mkataba lakini ilipigwa majungu mwishowe akanyanganywa gari.
“Nikaona sasa maisha yanazidi kuwa magumu, nikauza vyombo vyangu vya ndani vyote nilibakisha kitanda cha watoto tu, pesa nikaezeka nikahamia kwangu banda halina umeme wala maji, nimepata shida sana mimi” alisema kwa huzuni.
Mwisho akapata fikra ya kwenda bank kutafuta mikopo kutokana na shida kumchosha. “Nikenda bank kuomba mkopo sikupewa nikaambiwa sikopesheki mpaka niwe na hati ya nyumba, nikaunganishwa na tajiri mmoja naye akanambia miye nakukopesha pesa ununue gari, lakini ukishindwa kurejesha pesa zangu usinirejeshee gari nitachukua banda lako ambalo unaliweka dhamana, nilikubali cha ajabu sikupewa pesa ya kwenda kununua gari niipendayo niliambiwa tu kuna gari Darajani inauzwa nenda kaitizame ukiipenda nitailipia baada ya kuiona nikajibu tu nimeipenda ilimradi tu niipate lakini hata sikuipenda lakini ndio shida tena” alisema.
Na hapo ndio akapata gari na akaanza rasmi gari na tokea kuanza hiyo kazi sasa ni inafika mwaka wa sita anaendelea na kupakia wazungu na hataki kupakia waswahili kwa sababu anasema hawalipi.
Akaanza kutafuta kampuni za Tour wamsaidie mikataba awe dereva wao lakini hakupata mashirikiano kabisa akaanza kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari lakini hakupata msaada.
“Sikutegemea kama Habari zangu zilizokuwa zinaenea kuhusu miye na kazi yangu nilitumaini serikali ina masikio marefu itasikia kilio changu na itanisaidia lakini wapi, kimyaaa. Nimeenda wizara ya wanawake na watoto kuna mifuko ya mikopo ya kuwezesha wanawake wajasiliamali nimeandika barua ya maombi sijapata mpaka leo, inasikitisha” alisema.
0 Comments