Header Ads Widget

RAS NZUNDA "ONGEZENI KASI KWENYE MIRADI HII ILI ITUMIKE NA WANANCHI"

 


NA WILLIUM PAUL, MWANGA.


KATIBU Tawala mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya  Mwanga kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo majengo ya serikali na madarasa, ili ikamilike kwa wakati na kutoa huduma zenye tija kwa wananchi.


Nzunda alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo ambayo inatekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii.



Katika ukaguzi huo wa majengo ya serikali ya kutolea huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo ameagiza ujenzi huo ukamilike hasa majengo muhimu ili mwezi Novemba wananchi waanze kupata huduma za afya.


"Nasisitiza katika eneo hili la afya tuimarishe kuandaa watumishi katika utoaji wa huduma bora za afya,kazi yetu ni kujenga ustawi wa wananchi, serikali inapenda kuona matokeo ya uwekezaji uliofanyika na huduma zinazotolewa kwa wananchi ziwe na uwiano. " Alisema Nzunda.



Nzunda amepongeza miradi mingine ya ukarabati unaoendelea wa ofisi ya mkuu wa wilaya licha ya uwepo wa baadhi ya changamoto zinatatulika, ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi, ofisi za maafisa tarafa pamoja na madarasa na bweni katika shule ya sekondari Nyerere ambapo amehimiza wasimamizi hao kuendelea kushirikiana ili miradi hiyo ikamilike kwa haraka na kuzingatia ubora unaohitajika.


"Msiruhusu mtu anayekwamisha miradi hii ya maendeleo kwa kuchelewesha ukamilishaji wake kwani kutasababisha kupungua kwa ubora na tija ya maendeleo kwa wananchi, zingatieni maeneo ambayo yanalega ikiwemo ujenzi wa ofisi ya Kata ya Kigonigoni Tarafa Jipendea, hakikisheni wiki hii milango inawekwa" Alisema Nzunda


Aidha alitoa wito kwa waalimu kutobweteka na ubora wa majengo wakasahau majukumu yao kwani wao ndiyo watakaobadilisha maendeleo ya taaluma ya shule husika baada ya serikali kuboresha mazingira ya ujifunzaji shuleni huku akiwataka watendaji na watumishi kutoa kipaumbele kwa waalimu wanapofika ofisi za Halmashauri, Wilaya na mkoa ili warudi kuwahudumia wanafunzi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mwajuma Nasombe  alisema kuwa amepokea maelekezo ya kiongozi huyo na kuahidi kushirikiana na watendaji wenzake kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati ili iwe na matokeo chanya kwa wananchi.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI