Header Ads Widget

MADIWANI HALMASHAURI YA MOSHI WATAKA KUSHIRIKISHWA KATIKA UPANGAJI WA MIRADI YA BARABARA.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


MADIWANI wa Halmashauri ya Moshi wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wameitaka ofisi ya Wakala wa barabara vijijini (Tarura) kushirikiana na baraza la madiwani katika upangaji wa barabara vipaombele zitakazokuwa zikitengenezwa kwenye bajeti za mwaka wa fedha.


Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Moris Makoi wakati wa kikao cha baraza la madiwani cha kawaida ambapo alisema kuwa, zipo barabara ambazo ni kipaombele katika kujengwa kwake kukokana na kuwa katika hali mbaya lakini Tarura wamekuwa hawazioni.




"Sisi Madiwani ndio tupo karibu zaidi na wananchi na tunatambua barabara ipi ambayo ipo katika hali mbaya zaidi na inahitaji kufanyiwa ukarabati wa haraka lakini ninyi Tarura hamtambui hivyo ni vyema kabla ya kupitisha barabara ipi ijengwe kulingana na bajeti ya fedha mliyonayo mtushirikishe Madiwani ili tutoe ushauri" alisema Makoi.


Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo aliwataka Wakala wa Maji vijijini Ruwasa kutenga bajeti ya ukarabati pindi mabomba yanapokatwa wakati wa utengenezaji wa barabara ili kurudisha huduma mapema wananchi wasiteseke kwa kukosa huduma.



"Tunatambua sasa hivi yapo matengenezo ya barabara yanayoendelea lakini niwaombe Tarura ongeeni na wakandarasi wenu washirikiane na Ruwasa ili kuepuka uharibifu wa kukata miundombinu ya maji na pindi inapotokea basi Ruwasa mjitahidi kurudisha huduma mapema ili wananchi wasiteseke" alisema Makoi.


Akizungumza swala la hoja za mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) alisema kuwa, hoja zilizotolewa kwa Halmashauri hiyo zimesababishwa na Watumishi wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na ofisi ya Mkurugenzi kwa kukataa kusikiliza ushauri wa kamati ya fedha.



Mwenyekiti huyo aliitaka ofisi ya Mkurugenzi kubadilisha mfumo wa ufanyaji kazi pamoja na kupokea ushauri unaotolewa na Madiwani ili kuepuka kupata hoja zisizo na umuhimu.


Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita inaleta fedha nyingi za maendeleo na kuwaomba viongozi kuwa na utashi katika kusimamia fedha hizo ili miradi iweze kukamilika kwa wakati pamoja na kuzingatia thamani ya fedha.



Makori alitumia pia nafasi hiyo kuwasihi watumishi wa Halmashauri kuzingatia utaratibu wa ubadilishaji wa matumizi ya fedha kwa kufanya vikao vinavyohitajika ili kuepuka migogoro.


"Ofisi ya Mkurugenzi simamia kila Mtendaji wa kijiji, kitongaji na kata kujijengea tabia ya kufanya mikutano ya hadhara na kusoma taarifa za mapato na matumizi hii itapelekea wananchi kuwaamini na kuiamini Serikali yao" alisema Makori.

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI