MKOA wa Kilimanjaro umepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya shilingi Bilioni 350.502 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri saba za mkoa huo.
Bajeti hiyo ilipitishwa leo katika kikao cha kamati ya ushauri wa maendeleo mkoa (RCC) ambapo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa bajeti hiyo itachangia kukuza maendeleo ya mkoa.
Babu alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23 mkoa ulitengewa Bilioni 363.886 na hadi kufikia Februari mwaka huu mkoa umeshapokea Bilioni 222.183 ambapo Bilioni 55.411 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa kutoa fedha hizi katika mkoa wetu ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo" alisema Babu.
Alisema kuwa, katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 mkoa umepata mafanikio makubwa katika sekta ya Elimu kwa kuongezeka kwa viwango vya uandikishaji wanafunzi ikilinganishwa na miaka ya nyuma pamoja na kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, katika kipindi cha mwaka 2021/22 mkoa ulipokea Bilioni 42.5 kwa ajili ya kutekeleza miundombinu ya Afya 109 ikiwemo ujenzi wa kitengo cha mionzi na ukarabati wa kitengo cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.
"Upatikanaji wa dawa muhimu vifaa tiba na vitendanishi umeongezeka na kufikia asilimia 86 na nitumie nafasi hii kuzielekeza Halmashauri kusimamia utekelezaji wa miradi kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha za serikali" alisema Babu.
Kwa upande wa asilimia kumi kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenyeulemavu kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya Bilioni 1.139 zilitengwa na hadi kufikia Februari mwaka huu fedha zilizotolewa kama mikopo ni milioni 723.54.
Alisema kuwa jukumu la utoaji wa mikopo ni la kisheria na sio uamuzi wa mtu na kuzielekeza Halmashauri kuongeza kasi ya utoaji wa fedha hizo kwa wakati na kwa kuzingatia makusanyo ya kipindi husika.
Aidha Babu alisema kuwa, mkoa ulipokea tani 13175.65 za mbolea ya ruzuku kutoka Serikali kuu yenye thamani ya Bilioni 10.468 na tayari tani 7477.75 imeshatolewa kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema kuwa swala la utoaji wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani sio swala la kushauriana na wala sio swala la hisani bali ni swala la lazima.
Boisafi alisema kuwa, pia swala la kurejeshwa kwa fedha hizo kwa vikundi ambavyo vimekopesha ni la lazima ili fedha hizo ziweze kunufaisha vikundi vingine na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kikamilifu katika urejeshwaji wa fedha hizo.
"Niwaombe wakurugenzi na watumishi wa Halmashauri utoaji wa mikopo hii usiwe wa siri vikundi ambavyo vinapata mikopo vitangazwe kupitia kwenye mbao zetu za matangazo na kiasi walichopata ili kila mwananchi atambua kikundi kipi kimefaidika na kike hii ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasani" alisema Boisafi.
Mwisho...
0 Comments