Header Ads Widget

MAJUKUMU YA WAZAZI YANAYOPITILIZA CHANZO CHA WATOTO KUFANYIWA UKATILI

 

NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA

UBIZE wa wazazi umeonyesha kuwa ndio Sababu kubwa inayotajwa na inayopelekea watoto kufanyiwa Ukatili wa Kijinsia hasa ulawiti.


Katika karne hii ya 21 Wazazi na Walezi wameonekana wakitumia muda mwingi kazini na kusahau malezi ya watoto wao majumbani huku shughuli zote za malezi wakiwaachia wadada wa kazi na Bibi.


Hali hiyo imepelekea kushamiri kwa Vitendo vya Ukatili hasa Vitendo vya ulawiti kwa watoto wa kiume


Christer  Kayombo ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Mkoa Dodoma  anaeleza  sababu mbalimbali zinazopelekea makosa ya ulawiti ambayo ni pamoja na ukimya wa familia.


Anasema Familia nyingi zimekuwa zikiona aibu kuzungumza na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia  wakisema sio mila na desturi kuongelea mambo kama hayo hali inayopelekea kushamiri kwa matukio ya ulawiti kwa sababu watoto wamekuwa wakikosa taarifa au elimu kuhusu masuala ya ukatili.


Mzazi ndio mwalimu wa kwanza kama mtoto ataambiwa na mzazi wake juu ya ukatili inakuwa ni rahisi zaidi mtoto kusikia tofauti sauti ya mtu mwingine sauti ya mzazi inapenya kwenye masikio kwa haraka  kwa ufasaha na kwa makini kiufupi mtoto ana makinika kumsikiliza mzazi wake zaidi kuliko mtu mwengine.


“Sasa kama huyu mzazi anayetegemewa kuongea na Mtoto masuala ya ukatili katika familia halafu anakaa kimya inakuwa ni changamoto matokeo yake tunaona familia ambayo inakaa kimya haizungumzi masuala ya ukatili ni rahisi sana kupata watoto wengi wanaofanyiwa ukatili hususani kulawitiwa hasa watoto wa kiume, ”alisema mkuu huyo.


Anasema  masuala ya ukatili yamekuwa yakizungumzwa na nguvu kubwa ilikuwa imewekwa kwa watoto wa kike lakini sasa jamii inatakiwa kubadilika na kuelekeza jicho zaidi katika kuwalinda watoto wa kiume na tunaona mwimbi kubwa la watoto wa kiume wakilawitiwa hivyo watoto wa kiume hawako salama.


Anasema tunaona watoto hawa wanapokosa elimu sahihi kutoka kwa wazazi kinachotokea watoto hao wanapojifunza au kuona kwa watoto wao wanapoongelea masuala ya maadili au ya kingono na wanapotoshana masuala ya kulawitiana  sio kitu kizuri mzazi akiwa anatoa elimu hatoweza kufanya vitendo hivyo.


Sababu nyingine ni vibanda umiza(mabanda ya kuangalia senema na mpira) ambapo anaeleza  mtaani tunaona watu wakiwa wameweka vibanda au mabanda ya video ambapo wanaonyesha mipira lakini vibanda hivyo vimeonekana vikichangia kwa kiasi kikubwa watoto kulawitiwa kwani wamekuwa wakionyesha picha za ngono.


Sababu nyingine ni fursa ni namna gani mtu mzima anaweza kupata fursa kufanya kitendo cha ukatili ambapo tunaona mtu anayeweza kupata nafasi hiyo ni ndugu wa karibu Baba, Mjomba au bodaboda.


Matumizi ya simu  na baadhi ya tamthilia zinazoonyeshwa kwenye televisheni watoto hao wamekuwa wakiingia katika vitu vingi ambavyo havina maadili hali inayopelekea kwenda kujifunza wenyewe kwa wenyewe


MADHARA


Madhara ya ulawiti kwa watoto ni pamoja na kuambukizwa magonjwa yatokanayo na ngono ukimwi ,kaswende kisonono , fangasi na kuathirika kisaikolojia kwa watoto wanaofanyiwa ukatili kwani na wao wanaweza kuja kuwafanyia wengine huku wengine kujinyanyapaa wenyewe pale wanapokuwa wanaumwa.


Hata hivyo alitoa wito kwa jamii kuona mtoto wa mwenzio ni kama wako mtu mzima kuwa na hofu ya Mungu kuogopa  kumfanyia mtoto ukatili pia kuacha kufumbia macho vitendo hivyo kwani utakapotoa taarifa utakuwa umelinda watoto katika jamii na Tanzania kwa ujumla.


Hata hivyo anasema katika siku 16 za kupinga ukatili  jeshi la Polisi Dodoma kupitia mtandao wa polisi wanawake  Tanzania TPFnet  dawati la jinsia Dodoma na dawati makao makuu wamejipanga  kutoa elimu  kwa kupita mashuleni, nyumbani kwenye nyumba za ibada kwenye mikutano ya hadhara na vyombo vya habari kwa kufanya makongamano kushirikisha walemavu na kuandaa family gala lengo ni kutoa elimu juu ya masuala mazima ya malezi


Naye Mkurugenzi wa Binti Makini Foundation Janeth John amesema  ulawiti na ubakaji ni matukio yanayoumiza na yanatakiwa yachukuliwe hatua za kimkakati kutokana ukubwa wa matukio yalivyo  na madhara yake.


Anasema Wazazi na familia kuwa macho kwani matukio mengi yameonekana yakitokea majumbani pia katika karne yetu wazazi wameonekana wakielekeza nguvu kazini kwa kuwa bize na kazi na kusahau  uangalizi wa watoto.


Aidha anasema tumekuwa tukikaribisha wageni katika familia zetu bila kuangalia anayekaribishwa ni nani na ana madhara gani na tumekuwa tukiwakabidhi watoto wetu tukijua kuwa ni watu salama wakati ukweli ni kwamba hakuna usalama.


Anasema  matukio ya ulawiti ni mengi na yanatisha kwa sababu yanafanyika katika familia zetu na tumekuwa tukifumbia macho vitendo hivyo .


Anasema utakuta mtoto amefanyiwa ukatili na baba au mjomba na taarifa hizo hazitosemwa kwa kigezo ya kwamba ukisema utadhalilisha familia  na ndio maana matukio yanaendelea kushamiri kwa kiasi kikubwa huku mzazi kutomzingatia mtoto kapita wapi anachoangaliwa kikubwa mtoto amekula tu.


Anatoa ushauri kwa jamii kukemea vikali vitendo hivi vya ulawiti kwani tukikaa kimya baada ya miaka 10 au 20 ijayo tutakuwa na watoto  waovu kupindukia .


TAKWIMU


Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na jeshi la polisi zinaonyesha  Januari 2019 mpaka Machi 2022 jumla ya matukio ya ukatili yalikuwa 27838 ,ambapo ubakaji 19726 ,ulawiti 3260 huku wanaume waliolawitiwa walikuwa 3077 wanawake waliolawitiwa walikuwa 183.


Hata hivyo anasema katika kesi zote za ulawiti na ubakaji kati ya kesi 27838 zilizofanikiwa kufikishwa mahakamani zilikuwa 21013 na kesi zilizotolewa hukumu zilikuwa  14278 hivyo hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa.


Naye Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma  Mustapha Rajabu akiongea kwa niaba ya viongozi wa dini amesema kutokuwa na hofu ya Mungu ndio chanzo cha vitendo hivyo kuongezeka hali inayopelekea Mwenyezi Mungu kutuadhibu .


"Kama tunavyoona tunaadhibiwa kutokana na vitendo viovu tunavyofanya mfano mzuri  kwa Sasa nchi yetu tunaomba mvua hii inyeshe hii yote ni adhabu kutokana na matendo yetu maovu," anasema Shekhe Mustapha


Aidha amewataka Wazazi na Walezi kuwalea Watoto na sio kuwafuga kwa Maana kwamba kuhakikisha wanatoa mavunzo yaliomema kuanzia nyumbani ili Mtoto aweze kuwa na maadili mema


" Tuache kuwafuga watoto bali tuwalete katika njia na maadili sahihi Mtoto anapokuwa anatakiwa kufundishwa kwa kupewa adhabu lakini pia turudi katika maadili yetu na tuachane na  habari za Kuendeleza uzungu ," anasema Shekhe Mustapha


WANANCHI WALIKUWA NA HAYA YA KUSEMA


Hussein Hussein ni mkazi wa mailimbili kata ya miyuji na ni muhanga wa watoto wake walifanyiwa ukatili  huo aliiomba Serikali iangalie namna ya kulinda watoto kwa kuwa na njia mbadala ya kuzuia hali hiyo maana mkusanyiko wa watoto ni mkubwa na mambo haya yanaharibu jamii hasa pale kila wanaposikia Matukio hayo yakiongezeka kwa kasi .


“Tunaomba kuwepo na uongozi wa kusimamia masuala haya kwa nguvu maana uongozi wa chini hauna nguvu unaweza mfuata Balozi, Mwenyekiti wa mtaa na akashindwa kutatua hivyo unakuta masuala haya yanaishia huku chini hakuna wa kuyasemea ili kudhibitisha,”anasema mwananchi huyo.


VIONGOZI WA MTAA WALIKUWA NA HAYA YA KUSEMA


Akizungumzia kuhusiana na Matukio ya ulawiti Balozi wa Shina namba 3 katika mtaa wa Mathias, Boniface Kadebe anasema katika mtaa wake hakujawahi kuwepo tukio la aina hiyo Ila alipata taarifa kuwa katika Mtaa wake Kuna Matukio Kama hayo yakiendelea kwa watoto.


Anasema alipopata taarifa hizo  aliitisha kikao na kuwakutanisha wazazi,Walezi pamoja na watoto walifanyiwa Vitendo hivyo .


"Tulipowahoji watoto hao tulikuja kubaini ni zaidi ya watoto 7 walifanyiwa na kuwafanyia wenzao Vitendo vya Kulawitiana," anaeleza


Lakini pia Kadebe anaenda mbali zaidi na kusema kuwa waliwahoji wazazi na ndipo walipobaini wapo baadhi hawaishi na wenza  wao walishaachana na kutengana na mazingira ya nyumba ni chumba kimoja kina pazia tuu hivyo wanapoingiza wenzao watoto huwa wanaona.


“Sasa anapoingia na mwenzake matendo yanayofanyika watoto wanaona hivyo malezi yamechangia kuharibu watoto kwani wengine waliseme huwa wanachungulia bibi na babu wakiwa chumbani.


Tumegundua kuwa hao wazazi wamechangia kuleta mmomonyoko wa Vitendo hivi na kama ni hatua kali lazima nao wachukuliwe, maana ni chanzo,”anasema Balozi.


Hata hivyo hivi karibuni katika  siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 kila Mwaka Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyotokea hasa katika maeneo ya shule na nyumbani.


Waziri Dkt. Gwajima, amewasisitiza watoto hao kutokuogopa na badala yake waonapo vitendo vya ukatili au viashiria watoe taarifa kwa watu wanaowaamini ikiwepo dawati la jinsia linalopatikana kwenye vituo vya Polisi.


”Wanangu, Baba akikukatili mwambie Mama na kama ni Mama basi mwambie Baba, au kama unaona huwezi kumwambia Baba au Mama basi mwambie mtu unayemwamini alisikika akisema Dkt. Gwajima.


Hata hivyo serikali kupitia Wizara yenye dhamana na Watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ikiwepo Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa Sambamba na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI