Na,Jusline Marco;Arusha
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi amewataka wakandarasi waliopewa kandarasi za ujenzi wa miradi inayoendelea kwenye halmashauri hiyo kuongeza kasi ya kufanya kazi ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kulingana na mikataba yao.
Mkurugenzi Msumi ameyasema hayo wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi katika sekta ya elimu na afya inayotekelezwa katika halmashauri hiyo ambapo amewasihi wakandarasi hao, kutambua kuwa miradi ya serikali ina muda maalum wa utekelezaji kulingana na malengo ya mradi.
"Serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kufanya kazi hizo kwani wapo walioomba wakakosa hivyo tumieni fursa hii mliyopewa kufanya kazi zenye ubora pamoja na kukamilisha kwa wakati ulio kwenye mikataba yenu, kinyume na hapo mtapoteza sifa na kuvunjiwa mikataba yenu". Amesisitiza Msumi
Aidha Mkurugenzi Msumi amezitaka kamati za usimamizi wa miradi hiyo ngazi ya jamii, kuwabana wakandarasi hao na kuhakikisha wanakuwa katika eneo la kazini wakati wote.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi Zahanati ya Mirongoine, Ibrahimu Lemeirudi licha ya kuishukuru serikali kwa kuwapa fedha shilingi milioni 50 za kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo, ameipongeza serikali kwa kutumia force akaunti, utaratibu unaowapa fursa wananchi kusimamia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Ameongeza kuwa utaratibu huo wa matumizi ya force akaunti unawapa fursa wananchi kuilinda miradi hiyo na kufahamu hatua zote za utekeleza na kuhakikisha hakuna ubadhilifu wala upotevu wa fedha na mali ya Umma.
"Serikali kutumia kamati za wananchi, inasaidia usimamizi wa karibu, tunafahamu hatua zote za mradi, kuanzi mikataba, manunuzi, mapokezi ya vifaa na utunzaji, matumizi ya fedha zote za ujenzi hadi kulipia huduma zote kwa usimamizi wa watalamu wa halmashauri,lakini zaidi wananchi tunatambua mradi huu ni mali yetu". Amebainisha Mwenyekiti wa kamati.
0 Comments