Header Ads Widget

UNFPA YASEMA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NCHINI VINAWEZA KUEPUKIKA

 


 NA THABIT MADAI, ZANZIBAR –MATUKIO DAIMA APP

 SHIRIKA la Kimataifa la idadi ya watu Duniani UNFPA limesema asilimia 98 ya vifo vitokanavyo na uzazi nchini vinaweza kuzuilika endapo kutahimarishwa huduma muhimu za afya ya uzazi.

 

Meneja program ya Afya ya uzazi UNFPA Tanzania, Felista Bwana, aliyasema hayo katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari kuelekea kongamano la uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa mkutano wa idadi ya watu na maendeleo ambapo warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa hoteli ya Maru Maru Mjini Unguja.

 

Alisema, hatua hiyo pia itasaidia uwezekano wa kupungua idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu.

 

Alisema miongoni mwa hatua hizo ni kuwepo upatikanaji wa dawa sahihi na huduma za haraka zikiwemo kuongezwa ujuzi kwa wakunga na kuongezwa kwa huduma za dharura.

 

Aidha alisema ni vyema kwa wadau kuelekeza elimu ya afya ya uzazi kwa wakunga wa kienyeji ili kuona idadi ya vifo vinapungua nchini sambamba na kuongeza watumishi wa afya pamoja na vifaa tiba katika vituo vya afya.

 

Alisema, Tanzania imekuwa na changamoto ikiwemo maamuzi ya ngazi ya jamii na familia kuwa mzazi ili afike kwenye kituo cha afya baba atoe ruhusa jambo ambalo linasababisha kuengezeka idadi ya vifo.


Nae, mchambuzi wa masuala ya idadi ya watu na maendeleo kutoka UNFPA, Ramadhan Hangwa, alisema serikali inapaswa kutafuta namna bora yakupatikana kwa uhakika huduma muhimu za kijamii ikiwemo elimu ,maji na afya kutokana na kuwepo ongezeko la idadi ya watu kila mwaka ambapo kwa Tanzania watu wapatao milioni 1 laki tisa na 75 huongezeka.

 

Alisema, pamoja na mafanikio yaliyopatikana Tanzania kumekuwa na ongezeko la vifo ambapo katika kila wazazi laki moja wanawake 556 wanafariki jambo ambalo eneo hilo limekuwa na changamoto.

 

Aidha alisema eneo jingine ni kuwepo mimba za utotoni, na kwa Tanzania kila watoto 100, 27 wanapata mimba wakiwa na umri mdogo, pamoja na ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji ingawa miaka 20 iliyopita  imeonekana kupungua.

 

 

Hivyo, alisema wadau mbalimbali wamekutana ili kuona changamoto hizo zinamalizika kwa wakati ambapo Tanzania ilishiriki na kuundwa kamisheni ya ufuatiliaji wa maazimio na ahadi ya maazimio uliofanyika Nairobi mwaka 2019 ambao ulipokea taarifa ya dunia ya utekelezaji wa ahadi zilizotolewa mwaka 1994 mjini Cairo,Misri.

 

Nae, Afisa wa Program za Jinsia wa UNFPA, Ali Haji Hamadi, alisema, Tanzania imejitolea kuona vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto na wasichana vinafikia 0 katika masuala ya ukeketaji wa wanawake.

 

Aidha alisema, shirika hilo, limekuwa na lengo la kuisaidia serikali kufikia malengo yake ikiwemo kuziwezesha ili kuona masuala hayo yanamalizika ikiwemo mila potofu kuondoka.

 

Mapema, Mratibu wa ufuatiliaji wa kongamano hilo, Saskia Schellekens, alisema miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika ripoti hiyo ni kupunguza idadi ya vifo vya uzazi hadi kufikia asilimia 0, ukatili wa kijinsia pamoja na kumuwezesha mwanamke.

 

Uzinduzi wa ripoti hiyo unatarajiwa kufanyika  Zanzibar  Novemba 10 ambapo miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni Afya ya Uzazi pamoja na ushirikishwaji wanawake katika nafasi za uongozi.

 






 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI