Teddy Kilanga ARUSHA
Mamlaka ya mapato nchini (TRA)imeendelea kuweka mikakati na miundombinu ya ulipaji kodi kwa wateja wake ili kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania bara na visiwani.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya utalii jijini Arusha,Naibu kamishna wa idara ya kodi za ndani,Swalehe Byarugabe alisema wadau wa sekta hiyo ni kundi muhimu katika walipa kodi wakubwa na wakati ambao linatoa mchango wake mkubwa katika kulipa kodi.
"Na hapa tupo katika mwendelezo wa kukutana na makundi ya walipa kodi lango likiwa ni kusikiliza changamoto wanazokumbananazo zikiwemo za kibiashara pamoja na kikodi,"alisema Byarugabe.
Aidha alisema serikali imeelekeza TRA kujaribu kukaa pamoja na walipa kodi ili wawasikilize changamoto na mwisho wa siku waweze kuzitatua nakuweza kulipa kodi zao kwa hiyari.
Naibu huyo alisema wamekuwa na taratibu za kusikiliza changamoto kwa makundi kwani kwa kufanya hivyo hali ya mapato nchini inazidi kuongezeka kwani hali hiyo ni matunda yatokanayo na ushirikiano baina ya TRA na wateja wake kutoka sekta mbalimbali.
Naye Kamishna wa bodi ya mapato Zanzibar,Yusuph Mwenda alisema ushirikiano waliyonao ni moja ya kurahisisha ukusanyaji wa kodi kwa wateja wake ambapo sekta ya utalii kwa upande wa Zanzibar ndio unaoendesha uchumi kwa zaidi ya asilimia 40 hiyo mahusiano ya watalii wa bara huwa wanamalizia Tanzania Visiwani.
"Na leo tumekutana jijini Arusha kuwasikiliza changamoto za wadau wa sekta ya utalii ambapo tutapata fursa ya kuwaeleza njia nzuri ya kurahisisha kufanya shughuli zao za utalii nchini kote bila usumbufu kwa pamoja na wageni wanaofika nchini,"alisema.
Nao baadhi ya wadau wa sekta ya utalii walisema mahali wanapoomba wafanyiwe marekebisho ni pamoja na mfumo wa ulipaji kodi pamoja na baadhi ya sera ambazo zimekuwa changamoto katika shughuli zao za utalii hiyo kupitia kikao hicho wataweza kuwaonyesha taswira kamili.






0 Comments