Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amewaonya makandarasi wote wa ujenzi waliosaini mikataba ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja katika mwaka huu wa fedha kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA na kuwataka kwenda kutekeleza kazi zao kwa mujibu wa mikataba.
Katika zoezi la utiaji saini mikataba hiyo Meneja wa Tarura mkoa wa Njombe mhandisi Gerlad Matindi amesema katika mwaka huu wa fedha miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 22 inakwenda kutekelezwa katika wilaya zote za mkoa.
Kwa niaba ya kamanda wa Takukuru mkoa wa Njombe Kamanda Akoheki Mbapila ambaye ni mkuu wa dawati la uzuiaji rushwa amesema taasisi hiyo itafuatilia utekelezaji wa miradi yote ya ujenzi na kuwachukilia hatua makandarasi wote watakaokwenda kinyume na mikataba yao.Baada ya utiaji saini wa mikataba hiyo mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amesema hayuko tayari kuona kazi zikiharibika ili hali kila mtu anafahamu wajibu wake na hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba huku akiwataka mameneja wa TARURA wilaya zote kusimamia kikamilifu kazi hizo.Wakizungumza kwa niaba ya makandarasi hao baadhi ya wawakilishi wa makampuni ya ujenzi akiwemo Danford Mfikwa wameahidi kwenda kutekeleza kazi kama mikataba inavyowataka.Kuchelewa kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini hususani barabara na madaraja kumekuwa kukisababisha malalamiko makubwa toka kwa wananchi ambao wanashindwa kusafiri na kusafirisha mazao na bidhaa mbalimbali jambo linalokwamisha ukuaji wa uchumi.




.jpeg)




0 Comments