WANAWAKE wameshauriwa kutumia fursa inayotolewa na Serikali ya mikopo ya asilimia nne ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kujiletea maendeleo ili kuondokana na utegemezi.
Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri alipokutana na wananchi na wanachama wa CCM tawi la Indonet kata ya Motamburu wilaya Rombo ikiwa ni ziara ya uhamasishaji wa zoezi la Sensa anayoendelea nayo mkoani hapo.
Alisema kuwa, katika bajeti ya fedha mwaka 2022/23 Serikali ya chama cha Mapinduzi chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ikiwamo mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
"Serikali imeonyesha ni jinsi gani inatupenda sisi wanawake kilichobaki ni sisi kuchangamkia mikopo hiyo kwa kuunda vikundi mbalimbali na kuvisajili ili kunufaika na fedha hizo zisizo na riba" alisema Zuena.
Akizungumzia swala la Sensa, Mbunge huyo alisema kuwa, Agosti 23 mwaka huu kutakuwa na zoezi la Sensa ya watu na makazi ambapo lengo la kufanya hivyo ni ili Serikali iweze kutambua inawananchi wangapi na kuwaletea maendeleo kulingana na idadi hiyo ya watu.
Alisema kuwa, wapo baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha zoezi hilo kuwa ni la kisiasa na kuwataka wananchi kuwapuuza kwani halina uhusiano wowote na Siasa.
"Ndugu zangu maendeleo yanagawanywa kulingana na idadi ya watu hivyo tukijitokeza kwa wingi kuhesabiwa tukawa wengi tutapata maendeleo makubwa kwani tutapata mgao mkubwa wa fedha lakini tukijitokeza wachache idadi ikawa ndogo na mgao wa fedha za maendeleo nao utakuwa mdogo niwaombe tusichezee hii fursa" alisema Mbunge Zuena.
Mbunge huyo anaendelea na ziara yake katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro yenye lengo la kutoa elimu juu ya umuhimu wa kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi pamoja na kuzungumza mafanikio mbalimbali yaliyoletwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani.
Mwisho...
0 Comments