Gabriel Kilamlya MBEYA
Teknolojia ya ufugaji samaki kwa kutumia njia ya kitalu nyumba yaani Green House inayotolewa na mfugaji toka Magoda halmashauri ya mji wa Njombe imeonekana kuwa kivutio kikubwa kwa watanzania wengi katika maonesho ya kilimo Nanenane yanayofanyika kifaifa jijini Mbeya.
Upendo Shari toka katika kijiji cha Magoda Halmashauri ya mji wa Njombe ndiye anayefanya maonesho haya jijini Mbeya pamoja na kutoa elimu juu ya ufugaji huo wa Samaki ambaye anasema hali ya hewa ya baridi ya Njombe imekuwa kikwazo katika ufugaji wa samaki hatua iliyomlazimu kubuni teknolojia hiyo.
Juu ya bwawa dogo la samaki mfugaji Upendo ametengeneza banda la kuku pia ambalo linasaidia kuongeza mbolea ambayo ni chaula cha samaki pamoja na kuongeza joto katika bwawa hilo.
Taknolojia hii imeripotiwa kumvutia makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dokta Philip Mpango kulazimika kutembelea banda hili la Halmashauri ya mji wa Njombe na kuelekeza halmashauri zote kueneza teknolojia hiyo kwa wafugaji wa samaki.
Aida Alex,Erasmos Moshi na Baltazar Kairo ni baadhi ya watanzania wanaotembelea mabanda ya nane nane jijini Mbeya ambao wanakiri kuwapo kwa bidhaa,mifugo na mbegu zinazowashawishi kujifunzi zaidi.
Mkuu wa idara ya mifugo na Uvuvi Halmashauri ya mji wa Njombe bwana Thadei Luoga anasema elimu ya ufugaji bora wa mifugo ambayo wamekuwa wakiitoa imesaidia sana kuongeza molari ya ufugaji bora kwa wananchi wao akiwemo mfugaji huyu wa samaki.
Tarehe nane mwezi huu wa Nane ndiyo kilele cha maadhimisho haya ya wakulima yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya ambapo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni wa heshima atakayeyafunga maonesho haya.
.
................................
0 Comments