Askofu Mkuu wa kanisa la Mennonite Tanzania,Nelson Kisare ameishauri serikali kupitia wizara ya elimu kuweka somo la maadili shuleni ili kuepuka vitendo viovu vinavyoendelea nchini ikiwemo mauaji.Mwandishi Teddy Kilanga MDTV Arusha
Akizungumza machi 20,2022 katika hafla ya kumweka wakfu Mchungaji Mary Yohana Yunga kuwa shemasi wa kanisa hilo,Askofu Kisare amesema serikali ikiweka somo hilo shuleni kuanzia ngazi ya msingi litasaidia watoto kukua katika maadili mema.
Aidha amesema mmomonyoko wa maadili unaanzia kwa baadhi ya watu wazima hadi wadogo kwani imekuwa ni changamoto katika Taifa ikiwa serikali imeweka mfumo wa kiapo cha maadili lakini hali hiyo haitoshi bali inatakiwa kuwepo kwa somo hilo maalumu.
"Maadili yamepungua katika Taifa ukiangalia vitendo vya kikatili vimeongezeka hasa mauaji ni vyema kanisa likatekeleza wajibu wao katika kuelimisha lakini pamoja na hilo ni vyema serikali ikaongeza somo la maadili katika mitaala ya elimu ili isaide kuondoa haya,"amesema.
Naye Mkuu wa wilaya ya Arusha,Said Mtanda amesema ni vyema taasisi za kidini zikasaidia kutoa elimu ya maadili kwani serikali pekee haiwezi kukabiliana na tatizo hilo.
"Hatutegemei mtoto ambaye amelelewa vizuri katika kanisa au msikiti awe mtovu wa nidhamu katika jamii hivyo ni vyema taasisi hizi za dini zikaendelea kuisaidia serikali katika kuwafundisha watoto maadili,"amesema Mtanda.
Kwa upande wake Shemasi Mary Yohana Yunga amesema anamshukuru Mungu kwa kuchaguliwa kuwa shemasi wa kwanza mwanamke katika kanisa la Mennonite Tanzania hivyo anaamini anaweza kuifanya kazi hiyo.
0 Comments