MADEREVA wa mabasi yanatoa huduma za usafiri katika mikoa ya nyanda za juu kusini Njombe , Mbeya na Ruvuma jana wamegoma kutoa huduma wakishinikiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutengua zuio la mabasi hayo kuingia stendi ndogo ya Ipogolo .
Wakizungumza na wanahabari kuhusiana na mgomo huo madereva hao walisema wapo tayari kulipa ushuru wa Halmashauri mara mbili kwa maana stendi kuu ya mabasi ya mikoani iliyopo Igumbilo ambako ni mwanzo wa safari na watakapoingia stendi ya Ipogolo kushusha ama kupakia abiria pia watalipa ushuru .
Kwani walisema sababu kubwa inayotajwa na uongozi wa Halmashauri ya kutoruhusu matumizi ya stendi hiyo ya Ipogolo ni kukwepa kuua stendi ya Igumbilo ambayo serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wa stendi hiyo jambo ambalo wao wapo tayari kuifanya stendi hiyo kuendelea kuingiza kipato cha Halmashauri kwa kulipa ushuru kama kawaida.
Alisema Obadia Sanga alisema kuwa hadi sasa wao wamekuwa wakitumia stendi ya Igumbilo ambayo ni stendi ya mkoa wa Iringa lakini daladala za Mafinga zimekuwa zikitumia stendi ya Igumbilo na stendi ya Ipogolo jambo ambalo kwao limekuwa likiwatesa kwani abiria wao wamekuwa wakichukuliwa na daladala za Mafinga na kwenda kuwafaulisha Mafinga kwa pesa ambayo ni ndogo kwao .
" Tunachoomba uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuturuhusu tutumie stendi ya Ipogolo kushusha abiria tunapotoka Mbeya ama Njombe na tunapokwenda mikoa hiyo tukitokea Igumbilo basi turuhusiwe kuingia Ipogolo kuchukua abiria wa mikoa ya nyanda za juu kusini " alisema
Kwa utaratibu wa sasa si tu wanateseka wao wenye magari bali ni utaratibu unaowatesa hata abiria ambao wanalazimika kwenda kushuka Igumbilo ndipo waende Ipogolo ama pindi wanapotaka kuondoka basi watumie gharama kubwa kwenda Igumbilo kutafuta usafiri badala ya kusubiri usafiri Ipogolo
Huku Wamiliki wa mabasi hayo walisema kuwa hawapo tayari kuingiza mabasi yao barabarani kama changamoto hiyo haitapatiwa majibu ya kueleweka maana wanahisi kuna siasa ndani yake alisema John Nyalusi .
Kuwa wao kama wamiliki walishapeleka malalamiko yao kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia mstahiki meya ila hawakujibiwa kutokana na kukosa muda wa kukutana na meya kwa mazungumzo ya changamoto hiyo.
Baadhi ya wasafiri waliokuwa wakitegemea usafiri huo kwenda mikoa ya nyanda za juu kusini waliomba uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na madereva kumaliza tofauti yao kwani wao abiria ndio wanaoteseka kwa mgomo huo .
Anna Samson alisema kuwa alifika stendi ya Igumbilo toka saa 11 asubuhi ili kusafiri kwenda mkoani Mbeya kwenye mazishi lakini hadi saa 5 asubuhi hakuweza kusasfiri zaidi ya kusubiri mabasi ya Dodoma ama kutoka Dar es salaam ili apande .
Hata hivyo madereva hao ambao walilazimika kuendesha mabasi yao bila kupakia abiria kutoka stendi ya Igumbilo zaidi ya Kilomita 5 hadi stendi ya Ipogolo kuegesha kando kando ya barabara kuu ya Iringa - Mbeya walizuiliwa na jeshi la polisi kuendelea kuegesha mabasi yao barabarani hapo kutokana na hali ya usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.
Mgomo wa madereva hao ni mwendelezo wa mgomo ulioanza wiki mbili zilizopita ambapo mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema kuwa watakutana na madereva na wamiliki hao ili kusikiliza kero yao na kuangalia jinsi gani ya kuifanyia kazi .
Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Moyo akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na mgomo huo alisema kuwa stendi inayotambuliwa ni stendi ya Igumbilo na sio stendi ya Ipogolo hivyo mabasi yote ynayofanya safari zake nje ya mkoa wa Iringa yanapaswa kutumia stendi ya Igumbilo na sio Ipogolo.
0 Comments