Header Ads Widget

MAAFISA TFS WATAKIWA KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA BAJETI VYA WAKALA

 

 


Mwandishi Wetu, Dodoma

 

Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wametakiwa kusimamia ipasavyo vipaumbele vitatu vya Wakala kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

 

Akifungua kikao cha kujadili bajeti ya TFS kwa mwaka ujao wa fedha jana Februari 02, 2022 kinachofanyika katika ukumbi wa LAPF mjini hapa, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kusimamia uhifadhi endelevu wa rasilimali ya misitu inayoonyesha utayari wa nchi kuwa na ikolojia stahimilivu,  ambapo lengo ni kuwa na misitu iliyotunzwa vizuri.

 

Alitaja kipaumbe kingine kuwa ni usimamizi mzuri wa rasilimali nyuki ambayo imeendelezwa ili kukidhi mahitaji.

 


"Lakini tatu tuweze kuwa na rasilimali fedha itakayotumika kuendeleza rasilimali hizi za misitu na nyuki na vilevile kutuwezesha kuchangia mfuko mkuu wa serikali na kuimarisha ushirikiano na jamii zinazotuzunguka," alisema.

 

Katika kikao hicho cha siku tano kinachohudhuriwa na maofisa 134 wa TFS kutoka makao makuu, kanda na mashamba 23 yaliyo chini ya Wakala huo, kamishna wa uhifadhi pia aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi wakitanguliza mbele masilahi ya Taifa.

 

"Tusijifunge sana, tutazame mambo kwa  upana wake.. tuwe na bajeti ya kuifanya kazi yetu kuwa rahisi, mfano unaweza kuweka bajeti ya kuchimba kisima ambacho kitatumika na wananchi lakini pia nyuki na wanayama wadogo wadogo walioko kwenye msitu husika wakapata maji," alisema.

 


Mapema katika hotuba yake ya ufunguzi aliwakumbusha wajumbe wa kikao hicho kuwa mchakato wa bajeti unapaswa kuwa shirikishi utakaowezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa mfumo wa kijeshi.

 

"Bajeti yetu inatakiwa iweze kutusaidia kutekeleza majukumu yetu kupitia mfumo wa kijeshi kirasilimali watu na mazingira mengine wezeshi ya makazi na vitendea kazi," alisema Profesa Silayo.

 

Awali, akimkaribisha kufungua kikao hicho, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Emmanuel Wilfred alisema pamoja na mambo mengine wajumbe watajikita kujadili kuunganisha bajeti kutoka kwenye kanda za wakala, mashamba na makao makuu.

 

"Tutaiweka katika mfumo mzuri wa upangiliaji na kuhakiki," alisema.

 


Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Matumizi ya Rasilimali, Salehe Beleko anawaasa maafisa hao kuzingatia miongozo yote waliopewa ikiwa ni pamoja na kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM, 2020 – 2025).

 

Kikao hicho kinahudhuriwa na maofisa wanaohusika na bajeti, ufugaji nyuki na makamishna wa kanda na makao makuu wa TFS

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS