Header Ads Widget

UTANI WA WAVIDUNDA NA WANGONI

Siku ya leo nilivutiwa kuandika jambo juu ya kabila la Wangoni, kwani nilijaribu kujiuliza swali, hivi kwanini kabila hili lina watani wengi? Katika uandishi wangu juu ya habari za makabila mbalimbali ya Tanzania, nimebaini kuwa Wangoni ndilo kabila pekee nchini Tanzania lenye watani wengi.Mwandishi Adeladius Makwega

Nilipata swali lengine hivi inakuwaje hawa Wangoni kama watashiriki katika kushindania nafasi kubwa ya uongozi wa taifa letu kwa kupitia vyama vikubwa vya siasa, ushindani wake utakuwaje? Kwa maana kila kabila ukilifuatilia utakutana na Mngoni kapita huko. 


Jambo hili lilinipa maswali mengi kwa kuwa Wangoni wana utani na makabila kadhaa. Nilipokuwa naandaa matini haya juu ya kabila la Wavidunda zilikutana na ndugu zetu Wangoni ndiyo maana, mwanakwetu nimeyasema hayo maneno katika aya zangu hizi tatu za mwanzo.


Wavidunda ni kabila linalopatikana kwa wingi katika Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro huku katika wilaya hiyo wakiwapo Wasagara ambapo inaaminika wote ni wakaazi wa asili wa eneo linalofahamika kama Vidunda jirani na mlima Kidodi.


Utani katika kabila hili unatazamwa upo kati yao na Wangoni na Wasagara, ikiaminika kuwa utani wa awali ni ule wa kuzikana  ambapo familia waliofiwa mara baada ya msiba ujumbe hufika kwa majirani wote, hukusanyika na kufanya shughuli kadhaa na tamati ya yote sanda huandaliwa na kumzika marehemu.


Utani unaonekana wakati wa kuandaa pombe, katika familia za Wavidunda lazima kuandaa pombe ya watani, kama kuna mitungi mitano ya pombe iliyotayarishwa basi mtungi kati ya mmoja hadi miwili huwa kwa ajili ya watani, kinyume chake watani watafika na kuichukua pombe hiyo na mitungi yote na kutokomea nao kama iwe pombe ya biashara au ya sherehe, pombe ya watani ni faradhi.

Kwa mujibu wa mila, mahakama ilikuwa ni mali ya chifu (Watawala na Waamuzi), hizi mahakama za kileo hazikuwapo. Kwa hiyo hata kama kesi hiyo ikienda kwa chifu hakukuwa na kesi kwa kuwa huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa jamii ya Wavidunda.


Wavidunda wana utani baina yao wenyewe kwa wenyewe, mathalani bibi na mjukuu wake wa kiume na babu na mjukuu wake wa kike. Pia shangazi ana utani na mtoto wa kaka yake, shangazi ndiye mwalimu wa kumfundisha mtoto huyo wa kaka yake namna ya kushiriki tendo la ndoa, kwani kufanya mapenzi kabla ya ndoa ilikuwa ni mwiko.


Katika somo hilo maneno kadhaa ya viungo vya siri yalitamkwa kama yalivyo ambapo mwalimu huyo yaani shangazi alikuwa akitoa somo hilo kwa mtoto wa kaka yake. Hapo palikuwa na utani baina ya shangazi na na mtoto wa kaka yake katika kufundishana somo hilo la uzazi.


Pale ndoa inapofanyika baina ya makabila watani basi ilikuwa ni wajibu wa bwana harusi kuwapa mbuzi dume familia ya bibi harusi na kwa kufanya hivyo huwa panavunjwa utani(utani unapinguliwa) lakini pia bwana harusi alitoa pesa inayoitwa magweka kumpa baba wa bibi harusi.


Je kabila la Wavidunda wanakuwaje watani na Wangoni?


WAFITI ni sehemu ya kabila la Wangoni ambalo waligawanyika kutokana na Chifu Zulu (Nkosi Zulu) waliweka makaazi yao huku Mahenge (Upogoroni). Wafiti walisafiri hadi Usagara chini ya uongozi wa Kutukutu. 


Lengo lake Kutukutu ilikuwa ni kulivamia eneo la Usagara ambalo lilikuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na maji mengi, eneo hilo lilijumuisha Uluguru, Ukaguru na Upogoro. Wakiwa Vitani Wangoni (Wafiti) hao walikutana na Sultani Maro wa Usagara. 


Wakiendelea kusonga mbele na kuteka maeneo, walifika katika mlima Vidunda ambapo hapo Wangoni walianza kazi ya kuukwea mlima huu taratibu, huku wakiwasaka wenyeji katika mlima huo. Walipofika eneo la Chonwe, Wangoni walipambana na Chifu Luanda ambaye alikuwa akiyaporomosha mawe kutoka mlimani huku yakiwakuta Askari wa Wangoni waliokuwa wakipanda mlima huo.


Katika eneo hili askari wengi wa jeshi la Wangoni walifariki. Wakati mawe haya yalipokuwa yakiporomoka kutoka juu yakiwa mawe makubwa makubwa. Wangoni walilia wakisema-Bambu Kutukutu ayowide, wakimaanisha kuwa kiongozi wao Kutukutu ameuumizwa vibaya. Katika vita hivyo Kutukutu alimaliziwa kwa kupigwa risasi na bunduki za Wavidunda.


Ili kuokoa uhai wa wapiganaji wengine wa Kingoni, ndipo Wangoni walisalimu amri na kukaa pamoja kutatua mgogoro huo. Kikao hicho cha suluhu ndicho kilicholeta utani baina ya Wavidunda na Wangoni hadi leo hii.


Utani huu baina ya Wavidunda na Wangoni mara zote huwa hauna lugha kavu(lugha ya matusi) lakini kidogo kidogo kumekuwepo na matumzi ya lugha hiyo katika baadhi ya mambo, kwa mfano Wavidunda huwaita Wangoni GOZO. Kwa lugha ya Wavidunda GOZO ni sigara ya asili. Kiutani GOZO hugeuzwa na kuwa (Hashakumu si matusi) GOVI ikimaanisha mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara.


Kwa kuwa Wangoni hawakuwa na mila ya kufanya tohara, Wavidunda wanawaita Wangoni GOZO/GOVI kwa kuwalinganisha na sigara ambayo haijakatwa vizuri na hilo ikilinganishwa na sehemu za siri za mwanaume ambazo hazijafanyiwa tohara.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI